Mwandishi Wetu
Rais John Magufuli |
SAA chache baada ya kuhutubia Taifa
katika maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
yaliyofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Rais John Magufuli ametangaza
msamaha kwa wafungwa 2,219.
Kwa
mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest
Rwegasira, wafungwa watakaofaidika na msamaha huo ni waliotumikia nusu ya
vifungo vyao, wagonjwa, wazee, walioingia na mimba au watoto gerezani na wenye
matatizo ya akili.
Rais
ametoa msamaha huo kwa mujibu wa Ibara ya 45 (1) (d) ya Katiba, jambo ambalo
limekuwa likifanywa pia na marais waliomtangulia hasa katika sherehe ya Muungano
na Uhuru.
Katika maelezo yake, Meja Jenerali
Rwagasira alisema wagonjwa watakaoachwa ni wenye virusi vya Ukimwi, kifua kikuu
na saratani ambao hali zao kiafya zimethibitishwa na mganga mkuu wa mkoa au
wilaya.
“Wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au
zaidi. Umri huo uthibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au wilaya,” alisema.
Alisema msahama huo hautahusu waliohukumiwa
kunyongwa, maisha, kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya,
rushwa, unyang’anyi na kukutwa na silaha.
Wengine ni wenye makosa ya kubaka na
kunajisi, kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, wizi, kutumia
vibaya madaraka, kuzuia watoto kusoma, utekaji watoto na biashara ya viungo vya
binadamu na ujangili.
“Wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi
na ubadhirifu wa fedha za umma, kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi
halali na wafungwa warejeaji wa makosa na wafungwa waliowahi kufungwa gerezani
hawatasamehewa,” alisema.
Alisema ni matarajio ya Serikali kwamba baada ya kuachwa watarejea katika
jamii kushirikiana na wenzao kujenga Taifa huku akiwaonya kutorudia makosa ili
kuepuka kurejea kifungoni.
0 comments:
Post a Comment