Waandishi Wetu
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, limepiga marufuku wanachama wa CUF, kufanya usafi wa mazingira kwenye ofisi
za chama hicho Buguruni.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Simon Sirro
alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kauli ya Mbunge
wa Temeke, Abdallah Mtolea kuomba kufanya usafi kwenye ofisi hiyo Aprili 30.
Alisema Jeshi hilo limetoa zuio kutokana
na sababu za kiusalama ambazo zinatokana na mgogoro wa muda mrefu unaoendelea
ndani ya chama hicho.
“Tunaomba kila mwanachama wa CUF au
mwananchi afanye usafi katika eneo analoishi au ofisini kwake, kwa vile kitendo
cha kukusanyika kwa wanachama hao kinaweza kusababisha uvunjifu wa amani,”
alisema.
Alisema sheria ya Jeshi la Polisi sura
namba 322 yenye mapitio ya mwaka 2002, inatoa mamlaka kwa Kamanda kutoa zuio la
mkusanyiko huo na kuwataka kutii sheria bila shuruti.
Kamanda Sirro alisema kamwe Polisi haiwezi
kuruhusu makundi hayo mawili kukutana eneo moja na tayari wamekutana na
viongozi wa chama hicho na kuzungumza.
Katika mazungumzo hayo kwa mujibu wa
Sirro, Jeshi la Polisi liliwashauri viongozi hao, Profesa Ibrahim Lipumba na
Maalim Seif Sharrif Hamad, mgogoro wao uendelee ndani ya chama na si nje, kwani
watasababisha ugomvi na vyombo vya Dola.
Juzi Jumuiya ya Vijana ya CUF
(JUVICUF), ilitangaza mchakato wa kusafisha ofisi hiyo kesho.
JUVICUF
pia ilitumia fursa ya kukutana na waandishi wa habari, kulaani kitendo cha watu
wanaotajwa kuwa kundi la Profesa Lipumba kuvamia mkutano wa waandishi wa habari
na kuwajeruhi.
Mwenyekiti
wa JUVICUF Taifa, Hamidu Bobali ambaye pia ni Mbunge wa Mchinga, ndiye aliyetoa taarifa juzi akisema wameandaa
utaratibu mzuri wa kuwezesha kila kijana mwenye nia kokote aliko Dar es Salaam
na maeneo jirani kufika Buguruni.
Bobali
alisema lengo na nia ya kwenda Buguruni kwenye Ofisi Kuu za chama hicho, ni
kufanya usafi tu na si vinginevyo, hivyo vijana walipaswa kuunga mkono.
Imeandikwa na Leonce Zimbandu na Suleiman Msuya.
0 comments:
Post a Comment