Wankyo Gati, Arusha
BAADHI ya wauzaji wa madini ya Tanzanite
mkoani Arusha, wamelalamikia uwepo wa madini bandia ya Tanzanite hali ambayo
imekuwa ikikwamisha soko la madini hayo.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa
wahanga wa utapeli huo Gidion Lekasho alisema kuwa yeye alinunua madini bandia
ya Tanzanite ya Sh. milioni 8.
Alisema kutokana na matukio hayo
kuendelea kila siku sasa ni wakati muafaka kwa wizara ya madini kulifuatilia
suala hilo hasa katika maonyesho ya madini ya vito yanayotarajiwa kufanyika
hivi karibuni.
“Katika kipindi cha hivi karibuni
kumekuwepo na tatizo la uwepo wa madini bandia ya Tanzanite hali mbayo inatajwa
kutishia soko la madini hayo, huku baadhi ya wauzaji wakipata hasara,” alisema.
Mjiolojia kutoka
Wizara ya Nishati na Madini Kanda ya Kaskazini, Salome Timanywa alisema
madini yanapochimbwa yana umbo lake, hivyo wao kama wataalamu wanatambua
kutokana na umbo la madini hayo.
Alisema wamejipanga vizuri ili waweze kukabiliana
na hiyo changamoto na kuwataka wauzaji kufika wizarani ili kuweza kubaini
madini feki na ambayo siyo feki.
Kaimu Kamishna wa Madini Kanda ya Kaskazini,
Adam Jumaa alikiri kuwepo kwa tatizo hilo la madini bandia na kueleza kuwa
katika maonyesho ya madini ya vito yatakayofanyika, tayari wana wataalamu wa
kuyatambua madini hayo.
0 comments:
Post a Comment