Leonce Zimbandu na Dalila Sharif
Kituo cha Mabasi Ubungo |
CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Yaendayo Mikoani (TABOA),
Umoja wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (UWADAR) na Chama cha Wamiliki wa
Malori (TAT), wamesitisha mgomo uliopangwa kuanza jana.
Aidha, wadau hao wa usafirishaji wametaka kupewa rasimu
ya kanuni iliyotafsiriwa kwa Kiswahili na kupelekwa kwa wadau ndani ya siku 14.
Mbali na hatua ya kusitisha mgomo pia wametaka rasimu
hiyo itenganishe makosa ya dereva na mmiliki wa gari, kabla ya kuwasilishwa kwa
wadau kutoa maoni yao.
Makamu Mwenyekiti wa Taboa, Abdallah Kiongozi alisema
hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano uliokutanisha
wadau hao, vyama vya usafiri na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na
Majini (Sumatra), Dar es Salaam jana.
Alisema waliitisha mgomo kutokana na rasimu hiyo kuonesha
makosa ya dereva kulipiwa na mmiliki, hali ambayo ilikuwa kinyume na taratibu
za ajira.
“Hakuna mgomo kuanzia leo (jana), hivyo madereva
waendelee kufanya kazi ili kusubiri marekebisho ya rasimu ya kanuni kwa ajili
ya wadau kujadili,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema baada
ya vyama hivyo kutangaza usitishwaji wa huduma ya usafirishaji nchi jana,
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa alifanya kikao
na vyama hivyo.
Alisema baada ya kikao hicho kilichofanyika jana
alikubali rasimu hiyo ibadilishwe kwa Kiswahili ndani ya siku hizo 14 na
kuwasilishwa kwa wadau.
“Tunaomba huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo
nchini ziendelee kama kawaida wakati Serikali ikiendelea kufanya marekebisho ya
rasimu hiyo iliyoandikwa awali kwa Kiingereza,” alisema.
0 comments:
Post a Comment