Grace Gurisha
Agnes Waya (Masogange) |
MSANII Agnes Waya, maarufu Masogange anatarajiwa
kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam leo
wakati kesi yake ya tuhuma za kutumia dawa za kulevya inapokuja kwa kutajwa na kuangalia
kama upelelezi umekamilika au la.
Masogange anatarajiwa kufikishwa mbele ya Hakimu Mkazi,
Wilbard Mashauri wa mahakama hiyo, ambaye ndiye anasikiliza kesi hiyo.
Mara ya mwisho kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo
hakimu huyo alimpa onyo mshtakiwa huyo baada ya kuchelewa kufika katika chumba
cha mahakama, hatua iliyofikiwa baada ya Wakili wa Masogange, Nictogen Itege
kuieleza mahakama kuwa mteja wake yuko njiani anakuja.
Taarifa hiyo ilisababisha, Hakimu Mashauri kumuhoji kuwa
mbona yeye yupo mahakamani? Akadai kuwa walipita njia tofauti ndiyo sababu
ikatokea kuwa mmoja kafika mwingine bado.
Hakimu Mashauri alisema mteja wake anatakiwa afuate
masharti ya dhamana na mamlaka. Hata hivyo, baada ya muda kidogo Masogange
alionekana katika viwanja vya Mahakama wakati kesi yake tayari ilikuwa
imeahirishwa.
Awali, akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali
Constantine Kakula alidai kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 katika maeneo
yasiyojulikana ndani ya Jiji la Dar es Salaam Masogange alitumia dawa za kulevya
aina ya Heroin (Diacety Imophine).
Katika shtaka la pili, Kakula alidai kuwa kati ya
Februari 7 na 14, 2017 mtuhumiwa huyo alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam
na kwamba alifanya makosa hayo chini ya kifungu cha 18 (a) cha Sharia ya Kupambana
na Dawa za Kulevya namba 5 ya mwaka 2015.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Masogange alikana na
yuko nje kwa dhamana ya wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh. milioni 10.
0 comments:
Post a Comment