Hussein Ndubikile na Joyce Kasiki
Rais John Magufuli |
KUFA kufaana. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais John
Magufuli kuamuru madaktari 258 kuajiriwa na Serikali baada ya uamuzi wake wa
kutaka wakaajiriwe nchini Kenya kugonga ukuta.
Uamuzi huo umekuja siku 32 tangu ujumbe wa Serikali ya
Kenya ukiongozwa na Waziri wa Afya Dk. Cleopa Mailu kuliwasili nchini na
kukutana na Rais Magufuli kwa madhumuni ya kuomba kuajiri kwa mkataba madaktari
500 wa Tanzania ili kupunguza uhaba wa Madaktari nchini, ombi ambalo
lilikubaliwa.
Kitendo cha Rais Magufuli kuridhia madaktari hao kuomba
ajira nchini Kenya kilizua taharuki nchini, huku wachambuzi wa masuala ya afya
wakisema si jambo sahihi kwa kuwa nchi inakabiliwa na uhaba mkubwa wa madaktari.
Lakini wakati taratibu hizo zikiandaliwa huku madaktari
hao wakianza kufanya maombi, wananchi na madaktari nchini Kenya walifungua kesi
mahakamani kupinga uamuzi wa serikali yao.
Mahakama nchini Kenya ilishindwa kuondoa pingamizi ya
kupinga Madakatri hao wa Tanzania kwenda kufanya kazi nchini jambo ambalo jana
Serikali imesema Rais Magufuli ametaka madaktari hao waajiriwe nchini na
kupangiwa vituo vya kazi haraka iwezekanavyo.
"Hatua hiyo imekuja baada ya pingamizi hilo
kushindwa kuondolewa wakati tarehe ya utekelezaji wa makubaliano mikataba ya
ajira ambayo ni Aprili 6 hadi 10 mwaka huu kupita hivyo kuilazimu Serikali
kubadili uamuzi wake," alisema Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Alisema Machi 18, Wizara hiyo ilitangaza nafasi za ajira
kwa Madaktari wa Tanzania kwenda kufanya kazi nchini Kenya na kwmaba mpaka
kufikia Machi 27, jumla ya maombi 496 yaliwasilishwa.
Waziri Ummy alisema baada ya kufanyika uchambuzi
ilibainika kuwa madaktari 258 walikidhi vigezo vilivyotakiwa kwenda kufanya
kazi Kenya vikiwemo vya baadhi ya uhakiki wa vyeti vya taaluma na vyeti vya
Sekondari, vyuo walivyosoma na kuhitimu masomo, sehemu ambazo waombaji
walifanya mafunzo ya vitendo, kutakiwa na umri usiozidi miaka 55.
Vingine ni usajili wa mwombaji katika Baraza la Madaktari
la Tanganyika pamoja na kutokuwa mtumishi wa Umma, hospitali teule za
Halmashauri na hospitali za mashirika ya hiyari wanaolipwa mishahara na
Serikali.
''Wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea kukamilisha utaratibu
wa ajira za Madaktari wake nchini Kenya ikiwa ni pamoja na kutangaza nafasi
hizo za kazi na kufanya uchambuzi wa maombi ya kazi, kuandaa hati ya
makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Kenya kuhusu ajira hizo
za madaktari na mkataba wa ajira kwa madaktari hao, wananchi (Madaktari) watano
wa Kenya waliwasilisha pingamizi mahakamani kuitaka Serikali ya nchi yao
kusitisha kuajiri madaktari kutoka Tanzania'' alisema Waziri Ummy.
Aidha, alisema Serikali itakuwa tayari kushughulikia upya
ombi la Serikali ya Kenya kupatiwa Madaktari 500, pale ambapo hakutakuwa na
vikwazo vya kuwapeleka Madaktari hao Kenya.
Aliongeza kuwa kufuatia uamuzi huo majina ya madaktari
husika na vituo watakavyopangiwa kazi yatatangazwa katika mtandao wa wizara
hiyo pamoja na wataalamu wengine wa afya 11 walioleta maombi yao na kukidhi
vigezo.
0 comments:
Post a Comment