Mwandishi Wetu, Dodoma
Profesa Palamagamba Kabudi |
WAZIRI wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi,
jana aligeuka kivutio na kuzua mjadala kuhusu Sheria ya Ndoa inayoruhusu
wasichana wenye umri wa miaka 14 kuolewa na wavulana kuoa.
Waziri huyo alivuta hisia za wabunge wakati wa kipindi
cha Maswali na Majibu Bungeni wakati akijibu maswali ya wabunge kuhusu sheria
hiyo ambayo ilipingwa mahakamani na Serikali kwa swali la msingi lililoulizwa
na Mbunge wa Songwe, Philip Murugo (CCM).
Profesa Kabudi alijibu swali hilo kwa kutumia mifano ya
makabila likiwamo analotoka yeye akisema haiwezekani kubadili mila na desturi,
imani ya dini na itikadi kwa sheria peke yake.
“Ni kweli ipo sheria ya ndoa mchakato wake unaendelea,
niseme leo kuna jambo ambalo haliko sahihi kwenye hiyo sheria, inaruhusu mtoto
wa kike kuolewa na umri wa miaka 14 na mtoto wa kiume kuoa akiwa na umri wa
miaka 14. Kifungu kile mwaka 1971 kiliwekwa ili kukidhi matakwa ya jamii mbili,
Wamasai na Mabohora,” alisema Kabudi na kuongeza:
“Ikifika wakati hali imebadilika umuhimu upo
tutalijadili. Umri wa miaka 14 si kwa msichana tu hata mvulana anaruhusiwa kuoa
kama Mahakama imeruhusu.
“Nami nakubali umri huo mvulana hajafika kuoa na msichana
kuolewa. Jambo hili linataka mwafaka wa kijamii kama ambavyo mwaka 1970 ilikuwa
ni muhimu kuwaangalia Wamasai na Mabohora ambao ni sehemu ya Tanzania. Lakini maadam
mchakato unaendelea, inshallah siku itafika na jambo hilo litapita.
“Mambo ya mila, desturi na itikadi hayataki haraka,
yanataka mwafaka. Kuna umuhimu sasa wa vyuo vyetu kufundisha ‘Legal
Anthropology’, huwezi kubadili mila, desturi imani ya dini na itikadi kwa
kutumia sheria peke yake, utakuwa unajidanganya,” alisema Kabudi na kufafanua:
“Mimi natoka kwenye kabila ambalo lina mila isiyo nzuri
ya ukeketaji. Sheria ipo, imezuia lakini kwa sababu bado ni suala la imani na
itikadi za watu, leo wamelihamishia kwa watoto wachanga.”
Alifafanua: “Sasa nazungumza kama Profesa wa Sheria, ni
hatari na Waitara Chacha anajua kuna mila na desturi za anakotoka leo, mimi
siafikiani nazo, lakini zinahitaji elimu, zinahitaji uelewa. Ni vigumu mtu
anayetoka nje ya eneo hilo kuelewa, kwamba mapenzi ni pamoja na kipigo.”
Kauli hiyo ya Kabudi ilimwinua Mbunge wa Ukonga, Mwita
Waitara (Chadema) kuomba kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Bunge, lakini Mwenyekiti
Mussa Zungu alimnyima nafasi huku Waziri huyo akiomba wakitoka wakazungumze
zaidi.
Mbunge huyo ni mmoja wa waliouliza maswali ya nyongeza
baada ya swali la msingi la Murugo.
Awali akijibu swali la msingi, Kabudi alisema kazi ya
kurekebisha sheria ni endelevu, ili kuhakikisha sheria zinaendana na mabadiliko
yanayotokea katika jamii.
Profesa Kabudi alisema: “Sheria za nchi hubadilika
kulingana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, kisiasa, kitamaduni, kisayansi na
kiteknolojia, jambo ambalo haliwezi kuathiri sheria zilizopo na kusababisha
zipitwe.”
Alisema katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali iliunda
Tume ya Kurekebisha Sheria ambayo ni chombo maalumu, chenye dhamana ya kufanyia
mapitio sheria zilizopo, ili kukidhi malengo na makusudio ya kutungwa kwake.
“Serikali imekuwa ikiwasilisha miswada ya sheria bungeni
ili Taifa libaki na sheria zinazochochea ukuaji wa uchumi, uboreshaji wa huduma
na ustawi wa jamii,” alieleza.
0 comments:
Post a Comment