*Wachumi wasema ni pamoja na Serikali ‘kuitupa’ sekta binafsi
Rais John Magufuli |
Fidelis
Butahe na Suleiman Msuya
WAKATI biashara zikikwama, benki zikiyumba,
baadhi ya viwanda kufungwa na vingine kupunguza wafanyakazi huku wananchi waliokopa
ili kupata fedha kusaidia kuendesha maisha wakishindwa kufanya marejesho,
wasomi nchini wamesema mambo hayo yanatokana na mfumo ‘mbovu’ wa ulipaji kodi
na kuyumba kwa sekta binafsi.
Kwa hali hiyo, wameshauri wananchi walioachishwa
kazi kutumia elimu yao kujiajiri, kujitosa katika kilimo na kuitaka Serikali
kushirikisha sekta binafsi katika shughuli zake na kuachana na utaratibu wa
kukumbatia kila kitu, kwa maelezo kuwa unasababisha fedha kutokuwa kwenye
mzunguko.
“Mtu anaweza kubambikiwa kodi… unajua Sheria ya Kodi inataka mtu akitajiwa kiasi
cha kulipa alipe tu hata kama si cha kweli. Ni lazima alipe robo tatu ya kodi
hiyo, ndipo akate rufaa jambo ambalo watu wengi wanashindwa,” alisema Dk
Christopher Awinia, Mkurugenzi wa Kituo cha Uchumi na Maendeleo Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania (OUT).
Tangu Rais Magufuli aingie madarakani
amekuwa akihimiza kila mtu kufanya kazi ili kujipatia kipato ambacho
kitamwezesha kulipa kodi halali.
Hali hiyo iliambatana na kupambana na
ufisadi, kufuatilia wakwepa kodi, kufuta posho na mikutano ya Serikali hotelini,
kudhibiti safari za ndani na nje ya nchi zisizo na umuhimu sambamba na fedha
zote za mashirika ama taasisi zake kuhifadhiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mikakati hiyo inayodaiwa na baadhi ya
wananchi kuwa ndio imesababisha ugumu wa maisha, ndio iliyotolewa mfano na
wachumi waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti.
Profesa Damian Gabagambi wa Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA) alisema: “Kwa sasa tunachokiona ni Serikali
kuonekana kutotaka fedha zake ziende kwenye mikono ya sekta binafsi. Tatizo
limeanzia hapo.
“Haitaki fedha ziende benki na kampuni
binafsi. Mfano Serikali inahamia Dodoma na kuhamisha vitu vyake, lakini
inatumia majeshi badala ya watu binafsi ambao watalipwa fedha zitakazoingia
kwenye mfumo.”
Alisema anachokiona sasa ni sekta
binafsi ambayo ndiyo inaajiri idadi kubwa ya wananchi, kukabwa shingo, “haya
matatizo yanayotokea yalitarajiwa. Hatuwezi kuyashangaa kama Serikali
haitaruhusu fedha zake kuingia kwenye mfumo.”
Alisema suluhisho ni Serikali kutumia
sekta binafsi na kulipa madeni wanayodaiwa na makandarasi ili fedha ziingie
kwenye mzunguko.
Alibainisha kuwa wapo wanaodhani kuwa
hali inayotokea sasa ni kubadilika kwa utaratibu wa kuendesha uchumi kutokana
na watu kuishi kwa kutegemea ‘dili’ ambazo kwa sasa zimeyeyuka.
“Wapo pia wanaodhani kuwa yanayotokea
sasa ni mambo ya mpito tu. Wapo wanaodhani uendeshaji wa uchumi kwa sasa ndio
uliozalisha matatizo haya,” alisema.
Profesa Gabagambi alisisitiza kuwa
katika mfumo ambao Serikali inabana matumizi, inapata faida kwa kukusanya kodi
zaidi na kupunguza mfumuko wa bei, lakini kinadharia kuna uhusiano wa wa karibu
kati ya kupunguza mfumuko wa bei na kuongeza tatizo la ajira.
“Ni matatizo mawili ambayo ni pacha,
lakini yanakwenda kinyume. Ukiongeza ajira huibuka mfumuko wa bei na ukidhibiti
mfumuko wa bei lazima litaibuka tatizo la ajira,” alisema msomi huyo.
Alisema umefikia wakati wenye elimu
kuitumia kujiajiri sambamba na wengine kujitosa kwenye kilimo, kuliko kusubiri
ajira kutoka serikalini na sekta binafsi.
Dk Awinia aliungana na Profesa Gabagambi
na kusisitiza kuwa katika ulipaji kodi
wa aina hiyo, wengi husimamisha biashara zao jambo ambalo linasababisha watu
kupunguzwa kazi.
Akitolea mfano kusitishwa kwa viwanda
kuzalisha vinywaji na kuweka kwenye mifuko ya plastiki maarufu kama viroba,
alisema: “Watashindwa kuajiri watu kutokana na hali mbaya ya kiuchumi. Serikali
inapaswa kuangalia sera iliyopo kama ina tija.”
Alisema ili kunusuru hali hiyo, Serikali
inapaswa kuwa na mjadala na wadau wa sekta binafsi ili kujua njia ya kutatua
changamoto ili mazingira ya kuwekeza na biashara kuwa mazuri kwa kuzingatia mwelekeo
wa Bajeti.
Akizungumzia kodi, Mhadhiri Mwandamizi
wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Godbether Kinyondo alisema suala la kulipa kodi halikwepeki
na kushauri wananchi kuelekeza nguvu zao kwenye ujasiriamali ili kuweza kumudu
hali ngumu ya maisha.
“Hakuna shaka kuwa usimamizi katika kodi
ndio sababu lakini hakuna jinsi kama ulikuwa unadanganya katika ulipaji kodi
sasa utailipa na unaweza kushindwa kuendeleza kampuni yako,” alisema.
Alisema asilimia kubwa ya
wafanyabiashara hawapo tayari kupata hasara, hivyo baada ya kubanwa katika kodi
wanachukua uamuzi wa kupunguza wafanyakazi ili wapate faida.
0 comments:
Post a Comment