*Ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji akitokea ACT-Wazalendo
*Akiuka
kauli yake Zanzibar mwaka jana kuhusu wapinzani
Mwandishi Wetu
Profesa Kitila Mkumbo |
AMEJIRUDI. Ndivyo kitendo cha Rais John
Magufuli kumteua Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo
kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kinavyoweza kutafsiriwa.
Profesa Kitila aliteuliwa jana kuchukua
nafasi ya Mbogo Futakamba anayestaafu.
Tafsiri kwamba Rais Magufuli amejirudi
inaweza kutumika kwenye tukio hilo kwa kurejea kauli aliyopata kuitoa akiwa
Zanzibar kwenye ziara ya kushukuru wananchi wa kisiwa hicho baada ya Uchaguzi
Mkuu, aliposema hakuna mpinzani atakanyaga ukuu katika Serikali yake.
Rais Magufuli alisema anamshangaa Rais
wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwamba pamoja na kushinda uchaguzi kwa
asilimia 92, ameweka wapinzani kwenye Serikali yake, lakini yeye hawezi kufanya
hivyo.
“Kusema ukweli anayoyafanya Rais Shein
yanaonesha ana moyo wa ajabu sana, mimi siwezi kuruhusu mpinzani akanyage
katika Serikali yangu,” alisema.
Lakini jana, taarifa kutoka Ikulu ilibainisha
kuwa Rais Magufuli amemteua Profesa Mkumbo kushika wadhifa huo akitokea Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Profesa Mkumbo anakuwa mpinzani wa pili
kupewa wadhifa ndani ya Serikali ya Magufuli, wa kwanza akiwa Dk Augustino
Mrema aliyeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Parole. Mrema ni Mwenyekiti wa
TLP.
Katika uteuzi wa jana wengine walioteuliwa
ni Dk Leonard Akwilapo ambaye amekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia, kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara
hiyo.
Kutokana na uteuzi huo, aliyekuwa Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo, Maimuna Tarishi anahamishiwa kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu (Bunge) kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Mussa Uledi ambaye
uteuzi wake umetenguliwa.
Aidha, Rais Magufuli alimteua Dk Ave
Maria Semakafu kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu kuchukua nafasi ya Dk
Akwilapo, kabla ya uteuzi huo Sekamafu alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo
Kikuu Shirikishi cha Afya na Sayansi cha Muhimbili (MUHAS).
Kwa mujibu ya taarifa ya iliyosainiwa na
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa wateule hao watakula kiapo mbele
ya Rais leo Ikulu Dar es Salaam kuanzia saa tatu asubuhi.
Profesa Mkumbo
Akizungumza na JAMBOLEO baada ya uteuzi
huo, Profesa Mkumbo alisema amepokea kwa mikono miwili uteuzi huo na kuahidi
kufanya kazi na Rais Magufuli kwa moyo mmoja.
Alisema ni kweli yeye ni mpinzani,
lakini amekuwa akifanya kazi UDSM kama mtumishi wa umma, hivyo kitakachopungua
kwa sasa ni kuachana na siasa ili kusimamia wizara husika.
“Nimepokea uteuzi huu kwa moyo mmoja na
naahidi kufanya kazi kwa nguvu zote kama nilivyokuwa hapa UDSM, ila siasa
itabidi nikae pembeni kwa sasa,” alisema.
Aidha, alipoulizwa kuwa uteuzi huo
aliujua au aliusikia baada ya kutangazwa na Ikulu, alisema hayo ni mambo ya
ndani na hawezi kuyazungumza huku akisisitiza kuwa amepokea nafasi hiyo na
atafanya kazi bila tatizo.
Kuhusu kauli yake ya Aprili mwaka jana
kuwa Rais asiteue wahadhiri wa vyuo vikuu kushika nafasi za utendaji ili kuwapa
nafasi ya kufanya utafiti na kutoa taaluma, alisema ni kweli hajabadilika ila
hana budi kupokea uteuzi huo.
“Huu utaratibu wa kuteua wasomi tu ambao
ni walimu na wanataaluma kutoka vyuo vikuu hasa UDSM, si mzuri maana Rais haoneshi
kuandaa wengine kuchukua nafasi zao, tuachwe wasomi tufanye kazi za kitafiti na
kitaaluma,” sehemu ya maneno ya Mkumbo Aprili 17, mwaka jana.
Pamoja na uteuzi huo kuhusu watu wengi
Profesa Mkumbo ndiye aliibua mijadala katika mitandao ya kijamii ambapo watu walijikuta
wakijadili na wengine kutoamini kuwa amepewa nafasi hiyo.
Mmoja wa watu ambao walituma ujumbe kwenye
mitandao ya kijamii ni Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye
alisema Mkumbo hakujua uteuzi huo kabla.
0 comments:
Post a Comment