Grace Gurisha
Hussein Ndama |
UPANDE wa Jamuhuri katika kesi ya kutakatisha fedha chafu
inayomkabili mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Hussein Ndama (44), leo unatarajia
kujibu hoja za upande wa utetezi kama hati ya mashitaka ina upungufu kisheria
au la.
Majibu hayo yanatarajiwa kuwasilishwa mbele ya Hakimu
Mkazi, Victoria Nongwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, baada
ya Ndama kulalamika kuwa hati hiyo ina dosari, hivyo kuomba itupiliwe mbali.
Mara ya mwisho kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo,
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shedrack Kimaro aliomba iahirishwe kwa sababu wakili
aliyetakiwa kujibu hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi anaumwa.
Upande wa utetezi uliwasilisha hoja kuwa hati ya mashitaka
ya mfanyabiashara hiyo ina upungufu wa kisheria, hivyo Mahakama iitupilie mbali
hati hiyo na mshitakiwa aachwe huru.
Ndama anakabiliwa na tuhuma sita ikiwamo ya kutakatisha
fedha haramu na kujipatia dola 540,390 za Marekani sawa na zaidi ya Sh bilioni
moja kwa njia ya udanganyifu.
Akitetewa na Wakili Hashimu Rungwe anadaiwa kuwa Februari
20, 2014 akiwa Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya alighushi hati ya kuuza
madini nje na sampuli ya madini kwa kuonesha kuwa kampuni ya Muru Platnum
Tanzania Investment Ltd imemruhusu kusafirisha makasha manne ya dhahabu yenye
uzito wa kilo 207 yenye thamani ya dola 8,280,000 zaidi ya Sh bilioni 16 huku
akijua si kweli.
Katika tuhuma za pili, mshitakiwa huyo anadaiwa kuwa
Machi 6, 2014 akiwa Dar es Salaam
alighushi hati kutoka ofisi za Umoja wa Mataifa Dar es
Salaam akionesha kuwa kilo 207 za dhahabu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo zilitarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru kwenda kampuni ya Trade TJL DTYL Ltd ya Australia na kwamba hazina
jinai yoyote.
Ilidaiwa kuwa Februari 20, 2014 alighushi nyaraka za
malipo zenye namba R. 28092 za Februari 20, 2014 kuonesha kuwa Muru ililipa
kodi ya dola 331,200 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya uingizaji
kilo 207 za dhahabu zenye thamani ya dola 8,280,000 zilizotoka Congo huku
akijua si kweli.
Ndama anashitakiwa pia kuwa, Februari 20, 2014 alighushi
bima ya kampuni ya Phoenix of Tanzania Assurance Ltd ya tarehe hiyo ikionesha kuwa
Muru iliwekea bima makasha manne ya dhahabu huku akijua si kweli.
0 comments:
Post a Comment