Abraham Ntambara
Jaji Mutungi |
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema
Msajili wa Vyama Vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ndiye chanzo cha yanayoendelea
ndani yake kwa kuasisi makundi maovu.
CUF imedai Msajili huyo ni chanzo cha
makundi ya mazombi, Mungiki, wavamizi, wabeba bastola na mapanga yaliyoshiriki
matukio ya utekaji wanachama, viongozi wao, hata watu wa chama hicho kupigwa visu
mahakamani.
Hata hivyo, alipotafutwa Msajili
kuzungumzia tuhuma hizo hakupatikana, lakini Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Monica Laurent alisema ofisi yake
haiwezi kusema lolote, kwani anachojua suala la CUF liko mahakamani na kinachosubiriwa
ni Mahakama kutenda haki.
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari
jana na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa chama hicho upande wa
Maalim Seif Sharif Hamad, Salim Bimani alimtaja Jaji Mutungi kuwa aliyesababisha
pia mlezi wa vitendo hivyo vya kihalifu ikiwamo kuvamiwa kwa Ofisi Kuu ya Chama
ya Buguruni Dar es Salaam Septemba 24 mwaka jana.
“CUF haikubaliani na inalaani tamko la
kinafiki la Jaji Mutungi na tunamtaka avunje ushirikiano hasi wa kuhujumu
chama alioujenga kati yake, Profesa Ibrahim Lipumba na Jeshi la Polisi,” alidai
Bimani.
Alitaja orodha ya matukio na dosari
katika tamko la Jaji Mutungi, akisema kiongozi huyo alifanya makusudi ili
kuchochea vurugu ndani ya CUF kwa kilichodaiwa kuwa ni kwa maslahi binafsi au
waliomtuma.
Alisema Jaji Mutungi amekuwa mfuasi wa
Profesa Lipumba na mkereketwa kuliko wana CUF wenyewe na kwamba, wakati timu ya
Profesa Lipumba inakiri kuwa Juma Mkumbi ni Mwenyekiti wa Wilaya ya Kinondoni
na Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, Mutungi hajui na hataki kukubali.
Aliongeza kuwa Jaji Mutungi alimwandikia
Mkuu wa Polisi–IGP, ampe ushirikiano wa kila hali Lipumba kila unapohitajika na
asikilizwe kwa kila anacholielekeza Jeshi hilo, akidai kuwa ushahidi wa
yanayoendelea hauhitaji tochi.
Alitaja matukio mengine kuwa ni pamoja
na Jaji Mutungi kufanikisha wizi wa fedha za ruzuku Sh milioni 369 na kwamba hilo
lilifanyika huku Mutungi akijua mwajibikaji katika masuala ya fedha ni Katibu
Mkuu.
Bimani alimshutumu pia Jaji Mutungi kuwa
alipanga na Profesa Lipumba kuundwa Baraza Kuu bandia kisha kuteua Bodi bandia
ya Wadhamini baada ya kuona kesi imewakalia vibaya mahakamani.
Alidai kuwa kutokana na hali hiyo, kwa
mtazamo wao Jaji Mutungi amepoteza hadhi ya kuwa Jaji na anaivunjia heshima
nafasi hiyo, kwani amepoteza uadilifu na kamwe CUF haitakubaliana na uovu aliouasisi
na kuusimamia.
Alisisitiza kuwa CUF haitakubaliana na Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa chochote kitakachokuwa kinyume na matakwa ya
sheria.
Aliongeza kuwa CUF ni taasisi imara ya
kisiasa nchini yenye viongozi makini, itakayoendelea kujenga uhusiano na
ushirikiano mwema na wadau wenye dhamira ya dhati ya kustawisha na kuchochea
misingi ya demokrasia ya kweli nchini, utawala wa sheria, kulinda na kutetea haki
za binadamu, amani na kuunganisha Watanzania wote.
0 comments:
Post a Comment