Mashaka Mgeta
Eusebius Nzigilwa |
ASKOFU Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es
Salaam, Eusebius Nzigilwa, ameonya dhidi ya vitendo viovu vinavyofanywa kwa
wasio na hatia, lengo likiwa ni kulinda dhamana walizokabadhiwa ukiwamo
uongozi.
Askofu
Nzigilwa alisema hayo juzi alipohubiri katika adhimisho la Misa ya Pasaka,
Wakristo nchini wanapoungana na wenzao duniani kukumbuka kufufuka kwa Bwana
Yesu Kristo.
Alisema
uovu dhidi ya watu wasio na hatia ulifanyika pia dhidi ya Bwana Yesu,
alipotatufiwa ushahidi wa uongo, lakini licha ya kutofanikiwa, aliuawa na
kufufuka siku ya tatu.
Kwa mujibu
wa Askofu Nzigilwa, tukio hilo linaashiria ukweli usiobadilika kuhusu wema kushinda
uovu, ikiwa ni moja ya mafundisho mengi yanayotokana na kuadhimisha sikukuu ya
Pasaka.
Alisema
mateso na kifo cha Bwana Yesu vilitokana na hofu ya makuhani na Wayahudi,
kwamba kutokana na kazi alizofanya, alitishia kuwapo kwao kwenye madaraka ya
kidunia, pasipo kujua kwamba utawala wake haukuwa wa duniani.
Askofu
Nzigilwa alisema hata katika dunia ya sasa, wapo watawala wanaoundia hujuma
watu wema, wakitaka kuwaangamiza ili kukidhi hofu zao na nia ya kulinda kuwapo
kwao madarakani.
Kwa mujibu
wa Askofu Nzigilwa, dunia haipaswi kuwa mahali mtu asiye na hatia anaangamizwa
ili kulipa maslahi ya watu wengine na kwamba uovu kama huo unapofanyika hata
kama ni katika kipindi cha mpito, lazima utashindwa.
Alisema ipo
haja kwa watawala na wenye dhamana kutambua karama tofauti zilizo kwa watu,
kwamba zinapotumika ipasavyo zinachangia ujenzi wa Taifa.
Pia alisema
jamii inapaswa kuishi kwa upatanisho hasa inapotokea kutokuelewana kati ya watu
wa pande mbili au zaidi.
“Kuna mtu
anaweza kusema, mimi siwezi kumsaheme kabisa yule, kama Yesu aliteswa hadi kufa
na akasamehe, wewe umetendwa nini kuliko yeye hata ushindwe kusamehe?” Alihoji.
Askofu Nzigilwa
aliasa watu kujiepusha na hulka ya kufurahia mahangaiko ya binadamu wengine na
kwamba kinachopaswa kufanyika ni kusaidiana ili kuondokana na kadhia zilizopo.
Kwa upande
mwingine, alisema watu wanaokabiliwa na mahangaiko wanapaswa kutokata tamaa,
bali kuwa na imani kwamba wakati utafika wa kupata matumaini mapya.
Alisema
binadamu anapitia njia mbalimbali ikiwamo kuhangaika, kukumbwa na shida ingawa
wakati mwingine hupata furaha.
0 comments:
Post a Comment