Joyce Kasiki, Dodoma
Wachimbaji wadogo |
SERIKALI imetoa ruzuku ya Sh milioni 460 kwa ajili ya uchimbaji wa madini
mkoani Kigoma katika miradi saba ya uchimbaji mdogo wa chokaa na shaba
inayomilikiwa na watu binafsi.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Medard Kalemani alitoa kauli hiyo
jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Josephine Genzabuke
(CCM).
Genzabuke katika swali lake alitaka kujua Serikali imechukua hatua gani
kuendeleza utafutaji na uchimbaji wa madini hasa ikizingatiwa kuwa mkoa huo una
madini mbalimbali yakiwemo ya chokaa, dhahabu na platinum.
Akifafanua hatua hiyo ya Serikali, Kalemani alisema fedha hizo
zilitolea kipindi cha mwaka 2015 na kati
ya miradi hiyo, mitano ni miradi ya chokaa na ipo katika wilaya za Uvinza, Kasulu
na Kibondo.
Alisema Serikali imeendelea kutoa elimu ya uchimbaji salama, matumizi
bora ya baruti, utunzaji wa madini na kuboresha mazingira, pamoja na elimu ya
fursa ya biashara ikiwemo upatikanaji wa mikopo ya masharti nafuu.
Kwa sasa alisema Serikali inaendelea kutoa huduma za ugani kwa
wachimbaji wadogo wa madini na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya
madini, ili uwekezaji huo uwanufaishe Watanzania na kukuza pato la Taifa.
Katika swali la nyongeza Mbunge huyo alitaka kujua kama
Serikali inaweza kusaidia wananchi wa eneo la Kakere kijiji cha Kakonko, kuwa
wachimbaji rasmi wa madini ya chokaa badala ya kuwazuia kuchimba madini hayo
kama inavyofanyika hivi sasa.
Pia alitaka kujua mpango wa Serikali wa kutenga eneo la wachimbaji
wadogo wa chokaa ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea baadaye.
Akijibu swali hilo, Kalemani alisema Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na Sheria
ya Mazingira inasema mtu yeyote anaweza kumiliki eneo la uchimbaji na kwa
kutekeleza hilo, wapo wananchi wamepewa
leseni za uchimbaji wa madini mbalimbali yakiwemo ya chokaa.
0 comments:
Post a Comment