Suleiman Msuya
Askofu Josephat Gwajima |
ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Josephat Gwajima amewashukia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mbunge wa Kawe,
Halima Mdee, huku akimuelezea msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nasib Abdul
(Diamond Platnumz) kuwa ni mfuasi wa kundi la Freemason.
Hata hivyo, amesema kutokana na msanii
huyo kuomba radhi amemsamehe, lakini akirudia atamfanya kuwa simbi.
Gwajima aliwashukia watatu hao jana
wakati wa Ibada ya Jumapili iliyofanyika katika kanisa lake lilopo Ubungo Dar
es Salaam.
Akizungumzia kuhusu kutekwa kwa Ibrahim
Mussa maarufu (Roma Makatoliki) wenzake, Gwajima alieleza kuwa aliyesema Roma ataonekana
kabla ya Jumapili, ndiye anapaswa kueleza ni nani aliyemteka msanii huyo.
Gwajima alisema aliyevamia Studio ya
Tongwe ni wale wale ambao walivamia Studio za Clouds, hivyo si jambo la
kunyamazia.
“Ni nani anayeteka watu, anatumwa na
nani, anafanya kwa manufaa ya nani? Wa kuniambia ninyamaze hayupo kwani nikinyamaza
Mungu atainua mawe,” alisema Gwajima.
Alisema watu wengi wanaangalia hayo
hawataki kusema kwa sababu yeye anasema lakini itafikia mahali radio,
televisheni, mitandao na Tanzania itasema kwa sababu saa ya bwana itakuwa imefika.
“Sisi tunapambana na misukule iliyokufa
sembuse wewe mtekaji ndio maana nawaambia waliovamia studio Clouds ndio wale
wale waliovamia na kumteka Roma Mkatoliki,” alisema.
Alisema utekaji huo umefanywa na mtu
mmoja ndio maana jeshi la polisi limetaka aulizwe ambaye alisema atapatikana
kabla ya Jumapili.
“Ndugu zangu hebu mtingishe mwenzako
muulize una akili hivi mtu akipotea Jumatano halafu ukawaambia watu atapatikana
kabla ya Jumapili maana yake unajua alipo, una majeshi utamfuatilia alipo,
umemficha wewe na lalalalalaaa huyu Bashite anaiaibisha nchi, Sirro anasema
muulize yeye, tujiulize kama anawachukua atawachukua lini na saa ngapi, mtazame
muambie ajiandae,” alisema.
Gwajima alienda mbali na kusema ziro
kwenye makaratasi ndio inatafsiri namna ya kufikiri, kuzungumza na kutenda
hivyo yanayotokea ni ushahidi tosha.
Alisema yeye hana mpango wa kuhama nchi
na atakuwepo hapa kuhakikisha kuwa anazungumzia jamii ya Kitanzania ili iweze
kufahamu haki zake.
Alisema habari ya mtu anaitwa Ben Sanane
hadi leo haizungumzwi na hajaonekana jambo ambalo si sawa huku matukio kama
hayo yakiendelea.
Gwajima alisema ni jukumu la wananchi
kumuombea Rais, viongozi na wananchi kwa ujumla ili kukabiliana na changamoto
zilizopo kwani hali ilivyo inatoa tafsiri mbaya kwa Rais.
“Nasisitiza kuwa ziro katika makaratasi
inatafsiri namna ya kufikiri, kuzungumza na kutenda,” alisema.
Halima
Mdee
Akimzungumzia Mdee, Gwajima alisema
wakati wa uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), mbunge huyo
alipotoka baada ya kutumia lugha chafu na kumtaka aombe radhi.
Gwajima alisema ni kweli Mbunge huyo
aliudhika ila maneno ambayo ameyatoa kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai si sahihi
kwani ni kiongozi wa muhimili.
“Halima ni mbunge wangu na
tunaheshimiana sana ila hili alilolifanya halikubaliki kwani Spika ni mtu
mkubwa sana hata kama Chadema haikutendewa vizuri ila Halima hilo jambo si sawa
ni kweli uliudhika jambo halipo sawa nenda ukaombe msamaha,” alisema.
Alisema akiwa kama mbunge anapaswa
kuangalia jamii inayomzunguka hata kama aliudhika anapaswa kufuata taratibu za
kuonesha hasira zake, lazima aoneshe mfano kwao kwa kusema na kutenda.
Gwajima alimtaka mbunge huyo kuomba
msamaha ana kama hatafanya hivyo atampiga tena kwani ndio jukumu lake kama
kiongozi wa dini.
Diamond
Platnumz
Aidha, alisema Msanii Diamond Platnumz ni
mfuasi wa kundi la Freemason ila hatamchambua zaidi kwa ameshamwomba msamaha na
yeye amemsamehe.
“Almasi ingegeuka kuwa maji taka ila
nampa onyo kwani leo nilipanga nikupe video inaonesha kila kitu kuhusu kujiunga
na kundi hilo la Freemason,” alisema.
Hivi karibuni Diamond alidaiwa kutoa
wimbo unaoonyesha kumtetea mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam anayelumbana na
Gwijima kuhusu vyeti bandia na kuweka mistari inayomzungumzia askofu huyo wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima.
Gwajima alisema mtu yoyote ambaye
anasapoti vyeti feki hapaswi kuungwa mkono na mtu yoyote na kuwa iwapo Diamond
akirudia tena ataweka kila kitu wazi.
Alisema Biblia hairuhusu mtu akiomba
msamaha kupigwa hivyo yeye amemsamehe na kuwa akirudia hatakuwa na huruma naye.
0 comments:
Post a Comment