Leonce Zimbandu
Sophia Mjema |
WATENDAJI wa kata na mitaa wametakiwa kudhibiti ujenzi wa
makazi mabondeni ili kuiepushia Serikali migogoro na wananchi, ukiwamo ulitokea
katika bonde la Mkwajuni.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, alitoa rai hiyo kwenye
kilele cha Wiki ya Upandaji Miti katika kata ya Msongola mwishoni mwa wiki
iliyopita.
Alisema watendaji kushuhudia wananchi wakijenga katika
maeneo hatarishi na kushindwa kudhibiti mapema, ni tatizo sugu na kukosa uamuzi.
“Watendaji wanapaswa kuwajibika ipasavyo ili kuondoa kero
kwa wananchi ili mabonde hayo yatumike kupandwa miti,” alisema.
Alisema iwapo watendaji watawajibika vizuri, malalamiko
ya wananchi kuhusu migogoro ya ardhi yatapungua, ikiwamo ujenzi holela kwenye
vyanzo vya maji.
Mjema alitaka wananchi wahamasishwe na kupewa elimu ya
kutosha kuhusu umuhimu wa kutunza maeneo oevu kwa kupanda miti ya asili ikiwamo
mipingo, mininga na mivule.
Diwani wa Kata ya Msongola, Azizi Mwalile alisema
amefurahishwa na hatua ya Serikali kuteua sherehe za kilele za upandaji miti kwa
mkoa wa Dar es Salaam kufanyika kwenye kata yake.
Alisema hiyo ni heshima kwake, hivyo aliwataka wananchi
kupanda miti katika maeneo yao ili kunufaika nayo, ikiwamo kuvuna mbao, dawa na
kudhibiti saratani.
“Viongozi wa kata ya Msongola tumepata elimu ili kuhamasisha
wananchi kupanda miti katika maeneo yao,” alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya shule ya Msingi Yange yange,
Mrisho Goa alisema shule yake itakuwa mfano katika kata ya Msongola baada ya
viongozi wa mkoa kupanda miti siku hiyo.
Alisema anatarajia baada ya mwaka mmoja ugeni huo utafika
tena katika shule hiyo ili kukagua maendeleo ya miti waliyopanda.
0 comments:
Post a Comment