Mwandishi Wetu
Shamba la mpunga |
MASHAMBA ya mpunga matatu na skimu tatu
za umwagiliaji zimetozwa faini ya jumla ya Sh milioni 120.3 kwa ukiukaji wa
sheria za mazingira chini ya Baraza la Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC).
Mashamba hayo ni ya Mbarali Highland Estates,
Kapunga Rice Project na Kapunga Small Holders huku skimu za umwagiliaji zikitajwa
kuwa ni za Mwanavala (Nguvukazi), Mwashikamile na Mwendamtitu zilizoko Mbarali,
Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Mwenyekiti
wa Kikosikazi cha Kitaifa cha Kuokoa Ikolojia ya Mto Ruaha, Richard Muyungi,
alisema makosa yaliyokutwa katika mashamba hayo ni pamoja na kukosa vyeti vya
ukaguzi wa mazingira.
Lakini pia kukiuka taratibu za
umwagiliaji kwa kutoa na kutumia maji bila ruhusa, kuweka mifereji mikubwa ya
kumwagilia mashambani bila kufuata sheria na kanuni zinazotakiwa na
kutorekebisha miundombinu ya umwagiliaji kwa mifereji ya kutolea maji.
Faini hiyo inayotakiwa kulipwa ndani ya
siku 14 kuanzia juzi, ilitozwa na Kikosikazi hicho kupitia Mwananasheria wa
NEMC, Vicent Haule, baada ya kugundua makosa hayo ya uvunjifu wa sheria za
mazingira.
Kwa mujibu wa Muyungi Mbarali Estates inatozwa
Sh milioni 33, Kapunga Rice Project Sh milioni 33.1, Kapunga Small Holders Sh
milioni 3 huku Madibila ikitozwa Sh milioni 33.
Skimu za umwagiliaji za Mwendamtitu Sh
7,995,000, Mwanavala (Nguvukazi) Sh 7,995,000 na Mwashikamile Sh milioni 2.2.
Aidha aliongeza kuwa mashamba ya
Mwashikamile, Mwanavala na Kapunga Small Holders, wanatakiwa kulipa faini
lakini pia baada ya kuvuna watatakiwa kuacha kulima katika mashamba hayo mpaka
watapofuata taratibu za vibali vya maji na cheti cha ukaguzi wa mazingira
kutoka NEMC na Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji.
"Kutoza faini hizi si kukomoa mashamba
ila ni kuhakikisha kuwa wamiliki wa mashamba makubwa ya umawagiliaji nchini
wanafuata taratibu na sheria za mazingira katika kuendesha mashamba hayo,"
alisema Muyungi.
Kikosikazi hicho kiko Mbeya kukagua na
kutembelea sehemu za mashamba, skimu za umwagiliaji na kusikiliza maoni ya wananchi
ikiwa ni harakati za kurudisha ikolojia ya Mto Ruaha.
0 comments:
Post a Comment