Daudi Manongi, MAELEZO, Dodoma
Mikorosho mashambani |
SERIKALI itashughulikia malalamiko ya wakulima wa korosho
kwa kuondoa makato yasiyo muhimu kwenye zao hilo.
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William
ole Nasha alibainisha hayo wakati akijibu maswali ya wabunge jana akiahidi kuwa
Serikali itatekeleza hilo.
“Serikali imeshafanyia marekebisho maeneo ambayo wakulima
walikuwa wanalalamikia kwa kuondoa makato hayo kwenye zao hilo,” alisema Ole
Nasha.
Alisema Serikali imefuta ushuru wa Sh 20 kwa kilo kwa
ajili ya Chama Kikuu cha Ushirika, Sh 50 za usafirishaji korosho, Sh 10 kwa
kilo kwa ajili ya mtunza ghala na Sh 10 kwa kilo kwa ajili ya kikosikazi cha masoko.
Alisema sekta ya korosho ina utaratibu wa kupanga beidira
kwa kutumia vigezo vinavyokubaliwa kwa pamoja na wadau wote.
Kwa upande wa ununuzi wa pembejeo, alisema hufanywa kwa pamoja
na vyombo rasmi ndani ya sekta hiyo ambapo awali ilikuwa ikisimamiwa na Mfuko
wa Maendeleo ya Korosho na sasa Bodi ya Korosho Tanzania.
Alieleza changamoto zinazojitokeza katika kufikisha
pembejeo hizo kwa wakulima wa korosho na kwamba hatua zimechukuliwa kwa
kushirikisha vyama vya ushirika ili kudhibiti mianya ya pembejeo kwenda kwa
wasiolengwa.
Kwa mujibu wa Ole Nasha, Serikali imeweka mfumo wa
usambazaji pembejeo kwa lengo la kuhakikisha pembejeo hizo zinafikia walengwa
pekee.
“Utaratibu huu unazingatia kutambua wakulima wenye
uhitaji na pembejeo na hununuliwa kwa utaratibu wa ununuzi wa pamoja na kusambazwa
kwa wakulima kupitia wakala walioteuliwa na kuthibitishwa na Halmashauri
husika,” alisisitiza Ole Nasha.
0 comments:
Post a Comment