Suleiman Msuya
SHIRIKA la
Utafiti la Uwezo la Twaweza, limebaini kuwa miongoni mwa watoto wenye umri wa
miaka tisa hadi 13, wengi wao hawawezi kufanya majaribio ya kiwango cha darasa
la pili.
Kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa jana na shirika hilo kwa vyombo vya habari, takwimu hizo mpya
zinaonesha mwenendo mzuri katika somo la Kiswahili katika shule za msingi, huku
hali ya matabaka ikiendelea kujitokeza nchini.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze katika taarifa hiyo alisema katika takwimu
hizo wilaya ya Iringa Mjini, ilifanya vizuri kwa asilimia 74 ya watoto wenye
miaka tisa hadi 13 kufaulu majaribio ya kusoma Kiswahili na Kiingereza na
kufanya Hesabu.
Mkurugenzi huyo
alisema wilaya ya Sikonge, asilimia 15 pekee walifaulu ambapo kimkoa, asilimia
64 ya watoto wa Dar es Salaam wenye umri huo walifaulu majaribio yote matatu,
lakini mkoani Katavi asilimia 23 pekee ya watoto wenye umri huo ndio
waliofaulu.
“Vilevile,
asilimia 42 kutoka kaya masikini walifaulu majaribio yote matatu ukilinganisha
na asilimia 58 kutoka kaya tajiri. Tofauti hizi zinaonesha kuwa mahali anakoishi
mwanafunzi panachangia kwa kiwango kikubwa matokeo ya kujifunza kuliko hali ya
kiuchumi na vitu vingine ambavyo hudhaniwa,” alisema.
Kuhusu ufaulu,
alisema utafiti ulibainisha kuwa hali hiyo inatia moyo kuona watoto wanapata
matokeo mazuri zaidi kuliko miaka ya nyuma kwenye Kiswahili.
Alisema pamoja
na ufaulu huo, safari bado ni ndefu kwa kile alichodai kuwa ni kukosekana kwa
usawa kwenye matokeo ya kujifunza kuzingatia maeneo wanayoishi watoto.
“Takwimu zetu
zinaonesha kuwa mahali anakoishi mtoto huchangia kwa kiwango kikubwa uwezo wa
kujifunza, kuliko sababu zingine kama vile elimu ya mama, kupata ama kukosa elimu
ya awali au kuwa na udumavu au la.”
Alisema matabaka
yameendelea kujitokeza nchini ambapo alibainisha kuwa ipo tofauti ya asilimia
60 kati ya wilaya zinazofanya vizuri na zisizofanya vizuri
Alisema ripoti hiyo
inatokana na takwimu zilizokusanywa na Uwezo Tanzania ambayo ni sehemu ya
tathmini kubwa barani Afrika inayopima matokeo ya kujifunza ikiongozwa na
wananchi.
Eyakuze alisema
tathmini hiyo inatekelezwa pia Kenya na Uganda ambapo awamu ya sita ya
ukusanyaji wa takwimu uliofanywa na Uwezo Tanzania mwaka juzi, jumla ya watoto
197,451 walifanyiwa tathmini kutoka kaya 68,588.
Alisema takwimu
hizo zilikusanywa kutoka shule za msingi 4,750 na bado kiwango si kizuri kwa
ujumla ikilinganishwa na matarajio ya mitaala katika masomo yote matatu.
Aidha,
alibainisha kuwa takwimu hizo zinaonesha kuwa watoto wanaoweza kusoma hadithi
ya Kiswahili katika darasa la tatu ni asilimia 56 na la saba ni asilimia 89.
Alisema
wanaoweza kusoma hadithi ya Kiingereza, darasa la tatu ni asilimia 13 na la
saba ni asilimia 48, wanaofanya Hesabu ni asilimia 35 kwa darasa la tatu na la
saba ni asilimia 78.
0 comments:
Post a Comment