Celina Mathew
MVUA zinazoendelea
kunyesha zimesababisha vifo vya watu watatu baada ya kuangukukiwa na kifusi
kwenye machimbo ya mchanga ya Golani, yaliyopo Kigogo Fresh eneo la Pugu jijini
Dar es Salaam.
Marehemu hao wa umri
kati ya miaka 27-30, wawili wametajwa kwa jina moja la Amos na Shabani na mwingine
Boniface Pius, ambaye mwili wake bado ulikuwa ndani ya kifusi hicho hadi jana
mchana, huku Rashid Fadhili akijeruhiwa kwa kuvunjika mguu.
Akithibitisha kutokea
kwa ajali hiyo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alisema ilitokea
juzi tisa alasiri, ambapo mmoja alijeruhiwa kwa kuvunjika mguu na kwa sasa
anaendelea na matibabu.
Alisema marehemu hao wanatoka
familia tofauti na mpaka jana walishatambuliwa
na ndugu zao wakati uokoaji katika eneo hilo ukiendelea ili kubaini kama kuna
wengine.
“Taarifa ya kuwa kuna
watu wamekufa kutokana na kufukiwa na
kifusi ni za kweli wameshaopolewa na ndugu zao wameshawatambua kwa ajili ya
taratibu nyingine,”alisema.
Alisema mwili wa Pius
umeshindwa kuokolewa kutokana na udongo huo kuendelea kumong’onyoka na hivyo
kuleta changamoto kwenye uoakoaji, hali iliyowafanya kutafuta mbinu ya ziada
kwa kupeleka Excavator, ili kujenga njia itakayokuwa na kitu kizito
kitakachozuia udongo kuendelea kushuka.
Mkuu wa Wilaya hiyo,
Sophia Mjema alisema machimbo hayo yalifungwa miaka miwili iliyopita lakini
waliokuwa wakichimba walifanya kazi hiyo kinyemela.
Alisema shughuli hiyo
ilikuwa ikiendelea katika eneo hilo kinyume cha utaratibu kwa kuwa lilifungwa
hivyo wahusika walioruhusu watachukuliwa hatua za kisheria.
“Uchunguzi unafanyika
kubaini viongozi walioruhusu watu kuchimba eneo hilo wakati hairuhusiwi kwa
kuwa mchakato ulizuiwa siku nyingi na watachukuliwa hatua za kisheria kwakuwa
hatua hiyo imeleta madhara,”alisema.
0 comments:
Post a Comment