Fidelis Butahe
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC) kimesema juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano
kuhakikisha inapata suluhisho la kudumu la changamoto lukuki zinazolikabili
Taifa, haziwezi kufanikiwa kama inavyotakiwa bila kuwa na Katiba Mpya.
Kufuatia umuhimu huo wa Katiba, kituo
hicho kupitia Mkurugenzi wake mtendaji, Hellen Kijo Bisimba kimetoa mapendekezo
manne ya kuendelea kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya uliositishwa mapema mwaka
2015 kupisha uchaguzi mkuu.
“…Masuala mengi ambayo yamelalamikiwa na
wananchi na viongozi na hata juhudi za Rais Magufuli za kupambana na ufisadi,
kuirudisha heshima ya watendaji serikalini yangeweza kupata suluhisho kwa
kufufua mchakato wa Katiba Mpya ulioahirishwa bila tarehe maalum za
kuurejesha,” alisema Bisimba.
Wakati LHRC ikieleza hayo Machi 31 mwaka
huu Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi alisema Serikali
imeanza kupitia sheria zinazohusika na Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba kubaini
utaratibu mzuri wa kuendelea na mchakato huo kwa hatua ya kupiga kura ya maoni
kwa Katiba Inayopendekezwa.
Akieleza mapendekezo hayo, Bisimba
alisema lazima Serikali iboreshe sheria zinazoongoza mchakato huo, yaani Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83/2011 na Sheria ya Kura ya Maoni Na. 11/2013 ili
ziruhusu mwelekeo mpya wa mchakato huo.
“Maboresho haya ya sheria ni vema
yakazingatia kuondoa vifungu vibovu vya sheria hizo ambavyo vimekua kivuli cha
kuvurugika kwa muafaka katika hatua zilizopita za utungaji wa katiba mpya, ikiwemo
kupunguza uwezekano wa wanasiasa na vyama vya siasa kuuteka mchakato wa
Katiba,” alisema.
Alisema jambo la pili, wananchi wanapaswa
kudai kurudishwa mjadala wa kitaifa juu ya haja ya kufufua mchakato huo kwa mrengo
wa maoni ya wananchi na usitishwaji wa hatua inayofuata ya Kura ya Maoni kwa
mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni.
Alisema hali hiyo itatoa fursa kwa wadau
kujenga muafaka mpya wa kitaifa na kuamua namna bora ya kuendelea hatua
iliyobaki.
“Jambo la tatu ni Serikali kutenga
bajeti kwa mwaka 2017/2018 kuwezesha mchakato huu kuendelea,” alisema.
“Nne, Serikali itekeleze maagizo ya
hukumu inayohusiana na kura ya maoni iliyotolewa Februari 27 mwaka huu ili
kuweza kuifanyia mabadiliko sheria ya Kura ya Maoni namba 11 ya mwaka 2013
itakayotoa muongozo wa kuendelea na mchakato wa katiba.”
Alisema tangu kuanza kwa mchakato wa
Katiba mwaka 2011, zaidi ya Sh bilioni 1 zimetumika na kubainisha kuwa ni aibu
kutumia fedha nyingi kiasi hicho bila kupata Katiba.
“Kituo kinasikitishwa na ukimya wa
Serikali juu ya kuuendeleza mchakato huu. Licha ya Serikali kusema mchakato
utaendelea, lakini haikutengwa bajeti yoyote mwaka 2016/17,” alisema Bisimba.
“Kuwepo kwa kauli mbalimbali za viongozi
ambazo zinakatisha tamaa, bado hakujarudisha nyuma jitihada za wananchi kudai
mchakato huu kurejeshwa.”
Alisema pamoja na hatua iliyokwisha
kufikiwa, LHRC kinaamini bado kuna fursa na wajibu wa kufanikisha kufufua
mchakato huo ambao ulisusasua katika Bunge Maalum la Katiba baada ya baadhi ya
wajumbe kugoma kushiriki.
0 comments:
Post a Comment