Mwandishi Wetu, Tanga
WATU watatu
wamefariki dunia na wengine watatu kulazwa kwenye hospitali ya Kanisa la
Kinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Songe wilayani Kilindi mkoani hapa.
Kadhia hiyo
imetokana na kula uyoga unaodhaniwa kuwa na sumu nyumbani kwao kijijini
Mabalanga wilayani hapa, Aprili 22.
Kamanda wa Polisi
wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba jana aliwataja marehemu kuwa ni Rahma
Athumani (5) ambaye alifariki dunia usiku wa Aprili 22 baada ya kufikishwa katika
zahanati ya Mkuyu na kaka yake, Ramadhani Athumani (6) aliyefariki dunia siku
iliyofuata.
Ofisa Mtendaji
wa Kijiji cha Mabalanga, Ramadhani Maudo alisema jana kwa njia ya simu kwamba
mtu mwingine, Zaina Mbwana (36) alifariki dunia juzi mchana na kuzikwa
jana kijijini hapo kutokana na tatizo hilo.
Akizungumzia
tukio hilo, Kamanda Wakulyamba alisema tukio hilo lililohusisha watu wa familia
moja lilitokea siku hiyo, baada ya watoto hao kwenda porini kutafuta mboga na kuchuma
uyoga huo na walipofika nyumbani usiku, wazazi waliupika na kula.
"Inavyoonekana,
wazazi hawakutazama vizuri uyoga huo, walipoletewa na watoto wale, waliuandaa
na kuula ndipo walipojisikia vibaya na kukimbizwa kwenye zahanati ya kijiji cha
Mafleta kata ya Jaila, kwa matibabu na kuhamishiwa katika hospitali ya
KKKT," alisema.
Kamanda aliwataja
waliolazwa kuwa ni Mahija Athumani (9) ambaye anasoma darasa la pili katika
shule ya msingi Mabalanga, Mariamu Athumani (33) na Aziza Toba (13) ambao
wanaendelea na matibabu.
Alisema wataalamu
wa afya wanaendelea kuchunguza kujua aina ya sumu iliyokuwa kwenye uyoga huo
ambao watoto hao waliuchuma porini kama ilivyo desturi ya watu kula uyoga unaojiotea
porini.
Katika tukio lingine,
polisi mkoani hapa wanachunguza kifo cha Mariam Bernado (43) ambaye Aprili 21
alikutwa amekufa maji kwenye bwawa lililopo Handeni baada ya kutoweka nyumbani
kwao usiku.
Alisema mwanamke
huyo anayeishi nyumbani kwa mwalimu Gerard Moroma wa shule ya msingi Msasa,
alitoweka nyumbani usiku kabla ya kukutwa asubuhi akiwa amekufa bwawani humo ambalo
linatumiwa na wananchi wa Chanika.
Kamanda Wakulyamba,
alisema taarifa za awali za mama huyo zilisema alikuwa na matatizo ya akili
ambayo yanadaiwa kutokea baada ya kifo cha mumewe aliyemwachia watoto watatu
anaoishi nao kwa mwalimu huyo.
Katika tukio lingine,
mfanyabiashara Mohamed Ally (35) wa kijiji cha Mapanga tarafa ya Kwekivu
wilayani Kilindi amevamiwa na majambazi wenye bunduki aina ya magobori
wakimtaka awape fedha, lakini alipowaeleza hana, walimfyatulia risasi mbavuni
na kumuua.
Kamanda wa Polisi
alisema polisi inashikilia watu wanne kuhusu tukio hilo na pia wanaendelea kusaka
watu wengine waliohusika na tukio hilo.
0 comments:
Post a Comment