Juma Mohammed, MAELEZO Zanzibar
Ali Khalil Mirza |
KAZI ya
awali ya utafiti wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kwa
kutumia ndege maalum imekamilika visiwani Zanzibar, na sasa taarifa za utafiti
huo zimepelekwa Edinburgh Uingereza kwa ajili ya utambuzi wa kitaalam.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na
Mazingira Zanzibar, Ali Khalil Mirza, alisema kazi hiyo
imekwenda vizuri na watafiti hao walijiegemeza zaidi katika kitalu cha Pemba-
Unguja ambako waliruka kila siku kwa muda wa saa sita.
“Huu ni
utafiti wa awali, nachukua fursa hii kuwajulisha kwamba wataalam wetu
wamekamilisha kazi na wamefanikiwa kukusanya taarifa za kutosha kuhusu
rasilimali ya mafuta na gesi asilia hapa Zanzibar,” alisema Mirza.
Katibu
Mkuu huyo alisema awali kazi hiyo ilipangwa kufanyika kwa miezi
miwili, mwezi mmoja ndio utafiti wenyewe, lakini wakaweka na mwezi mwengine
ikiwa kutatokea dharura yoyote ambapo haikutokea na hivyo kukamilisha ndani ya
wiki tatu.
Kiongozi
wa timu ya watafiti kutoka kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya
Uingereza, Stefan Kuna alisema wamekamilisha kazi yao na kilichobakia ni
taarifa zilizokusanywa kuwasilisha Uingereza kwa ajili ya uchambuzi wa
kitaalamu.
Stefan
alisema kuwa wametumia wiki tatu kufanya kazi hiyo tofauti na makisio ya awali
ya miezi miwili, kutokana na kuanza kwa kipindi cha mvua za masika.
“Ndege
yetu ina vifaa ambavyo havihitaji vishindo, kama tutaruka wakati wa mvua na ngurumo
za radi, inaweza kurekodi kitu ambacho sisi hatukihitaji katika utafiti wetu ndio
sababu ilitulazimu kufanyakazi muda mrefu Zaidi,” alisema mtaalamu huyo.
Kiongozi
huyo wa timu ya wataalamu, alisema kazi yao ilikuwa kukagua miamba iliyoko
chini ya ardhi ambapo kwa kitaalamu inajulikana “Airborne Full Tensor Gravity
Gradiometry Survey” (FTG).
Stefan
alisema katika kitalu cha Pemba -Zanzibar wameona chembechembe ya mafuta, lakini
taarifa zaidi ya kuwepo kwa rasilimali ya mafuta na gesi asilia itapatikana
baada ya kukamilika kwa uchambuzi wa taarifa yao watakayoiwasilisha
Makao Makuu ya Kampuni ya Bell Geospace ya Uingereza.
Alisema
kazi ya uchambuzi wa taarifa za kitafiti walizokusanya itakamilika ndani ya
mwezi mmoja na wataikabidhi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Kampuni ya RAKGAS
ya Ras Khaimah, Falme za Kiarabu.
Mtaalamu
wa masuala ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta kutoka Kampuni ya ya RAKGAS ya
Ras Khaimah, Graham Cunningham ambaye pia ni Meneja wa Mkaazi wa RAKGAS
Zanzibar, alisema kimsingi kazi iliyoko mbele ni kubwa zaidi kwani huo ni
utafiti wa awali tu.
“Kuna
kazi kubwa mbele yetu, utafiti huu uliofanywa, utatusaidia kujua object iliyopo,
lakini kazi bado inaendelea,” alisema mtaalam huyo.
Alisema
katika miezi mitatu au mine, wanatarajia kuanza awamu ya pili ya utafiti kwa
kutumia meli maalum itakayofanya utafiti katika mwambao wa pwani ya Zanzibar
katika kitalu cha Pemba-Zanzibar.
Mtaalamu
huyo alisema pia utafiti huo utahusisha gari maalum litakalotafiti maeneo ya
ardhini katika sehemu ambazo taarifa zake zimetolewa katika utafiti wa awali
uliofanywa na ndege ya Kampuni ya Bell Geospace.
Kamapuni
hiyo ya kigeni inasaidiwa kazi na kampuni ya kizalendo ya Brunswick
Zanzibar Limited inayohusika na shughuli za uombaji wa vibali kutoka serikalini
kwa ajili ya ufanikishaji wa kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi
asilia Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment