Mwandishi Wetu
Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameomba viongozi wa dini
nchini kutumia nafasi zao kuhimiza wazazi na walezi kuishi maisha yenye
nidhamu, kuthamini kazi yenye kumpendeza Mungu, kusimamia malezi ya watoto na
kuzingatia maadili ya Taifa.
Waziri Mkuu alisema hayo jana wakati akifungua kongamano
kuhusu mmomonyoko wa maadili na athari za dawa za kulevya, lililoandaliwa na
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti
na Kupambana na Dawa za Kulevya, Dar es Salaam.
“Tabia na mwenendo mzuri ni lazima uanzie ngazi ya
familia, mtaani na hatimaye katika jamii. Tukirudia utamaduni wetu wa zamani wa
kusimamia maadili kwa pamoja, jamii yetu itanusurika kwa kiwango kikubwa,”
alisema.
Alisema kila mzazi au mlezi anapaswa kuona aibu, uchungu
na kujutia anapoona mtoto akienda kinyume na utaratibu wa kawaida wa maisha, na
ni vema wakatumia nafasi yao kuhimiza vijana waishi maisha ya nidhamu na yenye
kumpendeza Mungu.
Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kujenga jamii
yenye kuzingatia maadili nchini na kwamba Rais John Magufuli amekuwa akisisitizia
Watanzania kuzingatia maadili ya jamii kwa kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha
na rushwa na ubadhirifu.
Majaliwa alisema maadili kwa Taifa ni moja ya tunu muhimu
kwa kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha maendeleo, ujenzi wa umoja, amani,
upendo, uvumilivu na mshikamano kwa jamii.
“Hivyo hatuna budi nasi kulinda maadili hayo kwa uwezo
wetu wote, ili tuyarithishe kwa vizazi vijavyo, kama vile sisi tulivyorithi
kutoka kwa waasisi wa Taifa letu,” alisema na kuongeza:
“Hata hivyo, ninyi ni mashahidi kuwa katika siku za
karibuni tumeshuhudia vitendo vya mmomonyoko wa maadili na matokeo yake
yanaonekana dhahiri, kama kuongezeka kwa rushwa, kuiga utamaduni wa kigeni
ambao si mwema na hauna tija kwa jamii, na Taifa kwa ujumla.”
Alisema ni ukweli usiopingika kuwa mmomonyoko wa maadili
ni miongoni mwa vichocheo vya matumizi ya dawa za kulevya, hasa kwa vijana na
kwamba ni matarajio yake viongozi wa dini wataliangalia kwa kina tatizo hilo
ambalo kwa kiasi kikubwa linaathiri Taifa katika mipango yake.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema
Serikali iko mstari wa mbele kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za
kulevya nchini yanafanikiwa.
“Lengo ni kuhakikisha kuwa waathirika wote wa dawa hizo
wakiwamo vijana, ambao ni nguvukazi ya Taifa wanakombolewa dhidi ya janga
hilo,” alisema.
Alisema Serikali itashughulikia mtandao wa
wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na dawa za kulevya bila ajizi, ambapo
vyombo vyote vya kisheria vimeelekezwa kushirikiana katika mapambano dhidi ya dawa hizo kwa kusimamia sheria ipasavyo.
Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana
na Dawa za Kulevya nchini, Rogers Siyanga aliomba viongozi wa dini kuiunga
mkono Mamlaka hiyo kwa sababu inafanya kazi kubwa inayohitaji msaada wa watu
wote.
Mufti wa Tanzania, Alhaji Abubakary Zuberi alisema
viongozi wa dini nchini wana jukumu la kukataza maovu na kuiamrisha jamii
kufanya mambo mema badala ya kuiachia Serikali pekee kufanya kazi hiyo.
0 comments:
Post a Comment