Peter Akaro
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) |
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limemtaka Mwenyekiti wa
CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alaani kupigwa kwa waandishi wa habari wakati
wakitekeleza wajibu wao kwenye mkutano na viongozi wa chama hicho Kinondoni.
Limesema baada ya tukio hilo la Jumamosi iliyopita,
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliandika barua rasmi kwa uongozi
wa Jukwaa kulaani kupigwa waandishi hao na kutoa pole kwa walioumizwa na
kupata msukosuko.
TEF ilitoa tamko hilo lenye maazimio sita jana Dar es
Salaam mbele ya waandishi wa habari, wakiwamo waliopigwa kwenye mkutano huo
huku Mwenyekiti wake, Theophil Makunga akibainisha kuwa kupiga na kubughudhi
wanahabari hakupaswi kupewa nafasi.
Tangu tukio hilo, CUF ya Maalim Seif imekuwa ikidai kuwa
Profesa Lipumba na kundi lake, ndio waliofanya uvamizi huo, huku wakianika
picha za waliohusika kwenye tukio hilo katika mitandao ya kijamii.
Jumamosi takribani watu watano wakiwa katika gari lenye
nembo na bendera za CUF, walivamia mkutano huo kwenye hoteli ya Vinna,
Kinondoni na kupiga viongozi wa chama hicho na waandishi wa habari.
Miongoni mwa watu hao, mmoja aliyekuwa amejifunika uso na
kofia alichomoa bastola na kutishia huku mwingine akishindwa kuondoka baada ya
kuachwa na wenzake, jambo lililosababisha wananchi wamzingire na kumshushia
kipigo.
Katika maelezo yake, Makunga alisema tukio hilo
linaingilia uhuru wa habari kinyume cha sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016.
“TEF itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mikutano
ya Profesa Lipumba na wafuasi wake, tusiporidhika na hali ya usalama kwa
waandishi wa habari, tutalazimika kuchukua hatua zaidi,” alisema Makunga.
“Tunatoa mwito kwa wahariri na waandishi wa habari
kuchukua hadhari ya hali ya juu wanapoitwa kwenye kundi hili la kisiasa,” alisema
Makunga.
Alisema TEF pia ilitoa mwito kwa Polisi kuharakisha uchunguzi
wa tukio hilo na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika wa uhalifu
huo.
Aliongeza kuwa licha ya mgogoro unaoendelea ndani ya CUF,
vyombo vya habari vimekuwa vikitoa fursa ya kuandikwa na kutangazwa habari za
pande zote mbili zinazovutana.
Alisema kitendo cha watu au mtu kushambulia waandishi wa
habari walioalikwa kwenye tukio hilo, hakivumiliki na hakikubaliki.
Waandishi waliokumbwa na kipigo ni Fredy Mwanjala
(Channel Ten), Asha Bani (Mtanzania), Mary Geoffrey (Nipashe), Mariam Mziwanda
(Uhuru), Kalunde Jamal (Mwananchi), Rachel Chizoza (Clouds) na Henry Mwang’onde
(The Guardian).
0 comments:
Post a Comment