Celina Mathew
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati
na Maji (Ewura) imetangaza bei kikomo za mafuta.
Bei hiyo ya petroli imeshuka kutoka Sh 2,060 hadi Sh 2,057
kwa lita sawa na punguzo la asilimia 13 huku dizeli ikipanda kutoka Sh 1,913 hadi Sh 1,925 kwa lita sawa na
ongezeko la asilimia 12 ambapo bei hizo zinaanza kutumika rasmi leo nchi nzima.
Aidha, kutokana
na kupanda huko kwa bei, mafuta ya taa sasa yamepanda na yatauzwa Sh 1,858
kutoka Sh 1,852 ambayo ilikuwa bei ya awali.
Akizungumza Dar es Salaam jana kwa niaba
ya Mkurugenzi wa Ewura, Felix Ngamlagosi,
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Titus Kaguo alisema kushuka au kupanda kwa bei hizo za
mafuta ni kutokana na mabadiliko katika soko la dunia, mfumuko wa bei na
gharama za usafirishaji ikilinganishwa nba mwezi uliopita.
Alisema bei za jumla na rejareja kwa
petroli, mafuta ya taa na dizeli zimebadilika ikilinganishwa na toleo
lililopita la Machi mosi na kwamba petroli imepungua kwa Sh tatu sawa na asilimia
0.13. Aidha bei ya jumla imepungua Sh 5.65 kwa lita sawa na asilimia 0.29.
Pia bei ya rejareja kwa dizeli
imeongezeka Sh 12 kwa lita sawa na asilimia 0.63 ambapo bei ya jumla
imeongezeka kwa Sh 9.11 kwa lita sawa na asilimia 0.50.
Aidha, bei ya mafuta ya taa imepanda Sh
saba kwa lita sawa na asilimia 0.36 wakati bei ya jumla imepanda kwa Sh 3.68
kwa lita sawa na asilimia 0.21.
“Kwa kiasi kikubwa mabadiliko haya yanatokana
na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia, mfumuko wa bei na gharama
za usafirishaji tofauti na mwezi uliopita,” alisema.
Aliongeza kuwa Machi hakuna mzigo wa
mafuta uliopokewa nchini kupitia bandari ya Tanga na kwamba bei za rejareja za
mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka Sh saba kwa lita, sawa
na asilimia 0.32, Sh saba kwa lita sawa na asilimia 0.34, Sh saba kwa lita sawa
na asilimia 0.44 sawia.
Vilevile bei za jumla za mafuta ya
petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka Sh 3.68 kwa lita sawa na asilimia
0.19. Sh 3.68 kwa lita sawa na asilimia 0.20 na Sh 4.32 kwa lita sawa na
asilimia 0.28 sawia.
“Ongezeko la bei za mafuta linatokana na
ongezeko la faida ya wauza mafuta wa
jumla na rejareja kutokana na marekebisho yaliyofanywa kukidhi matakwa ya mfumuko
wa bei kwa mujibu wa kanuni ya ukokotoaji wa bei za mafuta katika mwaka 2016,” alisema.
Aidha, aliukumbusha umma kuwa bei kikomo
za mafuta kwa eneo husika zinapatikana kupitia simu za mkononi kwa kupiga
*152*00# kisha wafuate maelekezo na kwamba huduma hiyo inapatikana bure kupitia
mitandao yote ya simu nchini.
Kaguo alisema kwa mujibu wa sheria ya
mafuta ya mwaka 2015, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa
na soko, hivyo wao Ewura wataendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za
bei kikomo za bidhaa hiyo, kwa lengo la kusaidia wadau kufanya uamuzi stahiki
kuhusu ununuzi wake.
“Kampuni za mafuta ziko huru kuuza
bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani, mradi bei hizo ziwe chini ya
bei kikomo kama ilivyokokotoa kulingana na kanuni ya kukokotoa bei za mafuta zilizochapishwa
na Ewura na ambayo ilichapishwa na Gazeti la Serikali Namba 70/2016 la Februari
mwaka jana,” alisema.
Alivitaka vituo vyote vya mafuta
kuhakikisha vinabandika bei za bidhaa hiyo kwenye mabango bayana yakionesha
bei, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.
“Pale ambapo inawezekana kuchagua,
wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa
bei ndogo zaidi ili kushamirisha ushindani.
“Ni kosa kuuza mafuta bila mabango ya
bei bayana kwa wateja, adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza
matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika,” alisema.
Alitaka wanunuzi kuhakikisha wanapewa
stakabadhi ya malipo zikionesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta
yaliyonunuliwa na bei kwa lita ambapo itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa
mafuta, endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu
kuliko bei kikomo au yenye kiwango cha ubora kisichofaa.
0 comments:
Post a Comment