Suleiman Msuya
Makontena yenye mchanga wa dhahabu |
WAKATI Rais John Magufuli akiunda ya
kuchunguza taarifa za makinika ya dhahabu kutoka migodini kama una asilimia 90
ya madini hayo, wataalamu wamebainisha kwamba kiwango hicho kikithibitishwa, Tanzania
itakuwa imevunja rekodi ya kuzalisha tani 4,000 kwa mwaka, kiasi ambacho
hakijawahi kutokea tangu dunia iumbwe.
Aidha, wamesema ili kujenga kiwanda cha
kuchenjua dhahabu nchini takriban megawati 500 za umeme wa uhakika zinahitajika
kwa kiwanda kimoja jambo Tanzania haiwezi kulifanikisha kwa nishati iliyopo.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya
Rais kuunda tume hiyo kuchunguza mchanga kwenye kontena 282 alizobaini
alipotembelea bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni zikiwa katika mchakato wa
kusafirishwa.
Akizungumza katika kipindi cha Mizani ya
Wiki kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha Azam, Meneja Mkuu wa Uhusiano wa Serikali wa kampuni
ya Accacia, Assah Mwaipopo alisema Serikali ina haki ya kuhakiki, lakini
haiwezi kutokea yanayosemwa yakawa kweli.
Mwaipopo alisema katika historia,
inaonesha kuwa nchi inayozalisha dhahabu kwa wingi duniani ni Afrika Kusini
ambayo inazalisha tani 600 hadi 400 na kiwango cha dunia kwa takwimu za mwaka 2015
ni tani 2,500 tu hadi sasa.
Alisema wanaosema kuwa mchanga huo una
dhahabu asilimia 90 wanatoa tafsiri potofu na kubainisha kuwa hata miche ambayo
wanavuna katika hatua ya kwanza dhahabu si asilimia 90.
Meneja huyo alisema ni vigumu kutorosha
dhahabu hasa kampuni ya Accacia ambayo imesajiliwa katika Soko la Hisa la
London, Uingereza na kusisitiza kuwa taarifa hiyo itaondoa utata.
“Mfano ukisema kontena moja lina
asilimia 90 ya dhahabu ni kwamba kuna tani 18 za dhahabu katika kontena la tani
20; ni vigumu kwani kwa kontena 260 zilizo bandarini unataka kuiambia dunia bandari ya Dar es
Salaam ina tani 4,000, ni taarifa ya kushitua dunia,
“Haijatokea kwa mwaka mmoja dunia
ikavuna tani 3,000, kwani nyingi sana ni 2,500 hivyo taarifa zinazosemwa si
sahihi ila ngoja Serikali ijiridhishe,” alisema.
Mchakato
Mwaipopo alisema mchakato wa kuchimba dhahabu
una hatua muhimu ambazo zinahitajika ili kupatikana dhahabu ambapo katika hatua
ya kwanza dhahabu huwa kubwa.
Alisema katika hatua ya pili kemikali
zinazovuta dhahabu hutumika ili madini hayo kutenganishwa.
Alisema uchenjuaji unahusu tani moja ya
makinikia ili kupata gramu mbili, hivyo haiwezi kuwa kama inavyosemwa kwamba asilimia
90 ya mchanga huo ni dhahabu.
Mwaipopo alisema pia hutumia kemikali ya
carbon kupata dhahabu kabla ya kufikia makapi ila kama ingewezekana wangeishia kwenye
makinikia.
Alisema kemikali ya synite ni aghali na baada
ya matumizi inapaswa kuharibiwa hivyo ni ngumu kuiingiza nchini.
“Katika kuchenjua tunapata gramu 0.02
ambayo inatoka kwenye tani moja kwani yale ni makapi tunayaita dhahabu athari,”
alisema.
Alisema kibiashara ingekuwa heri
mchakato wa dhahabu kuishia kwenye makinikia ila gramu 150 kwa tani na
ukiibadilisha tani iwe gramu utapata gramu 0.02 kwenye wastani wa tani moja.
Mhandisi huyo alisema katika mgodi wa
Buzwagi wanapata tani 18 za shaba ambapo kwa gharama ya soko haina tija kubwa.
Kuhusu gharama za kusafirishia, alisema
si kubwa sana kwani kontena moja linasafirishwa kwa dola 2,000 za Marekani na
kuchenjua haizidi dola 1,000 hivyo tani 3.6 itakayopatikana itarejesha gharama
na faida.
Mahitaji
Akifafanua kuhusu kiwanda cha kuchenjua
dhahabu nchini alisema kiuhalisia kiwanda hicho kinahitaji uwekezaji wa muda
mrefu ambao utazingatia ukweli kuhusu makinikia yaliyopo.
Alisema uwezo wa migodi iliyopo nchini
ni kuzalisha makinikia tani zaidi 50,000 na kuwa ili kiwanda kifanye kazi yanahitajika
makinikia tani 150,000 kwa mwaka.
Mwaipopo alisema pia kiwanda kimoja kitahitaji
umeme wa megawati 500 hivyo kwa Tanzania ni vigumu kupata umeme huo kwani
uliopo ni wa megawati 2,000.
“Kama yupo mwekezaji anayetaka kuwekeza
anakaribishwa, lakini ni vema akahakikishiwa uendelevu wa uwekezaji wake kwani
kiwanda kinachofanya kazi hiyo ya kuchenjua makinikia kina thamani ya zaidi ya
dola milioni 500,” alisema.
Alisema mgodi wa Buzwagi umeanza kwisha
hivyo utakaobaki ni Bulyanhulu jambo ambalo linaweka bayana kuwa makinikia
yatakuwa tani 30,000 kwa siku zijazo.
Mtaalamu
Dk Elisante Mshiu alisema dhahabu ni
dhahabu wakati unatumia ila kijiolojia inapatikana kwenye ukanda wa miamba.
Alisema Tanzania ina kanda sita ila kanda
ya Ziwa Victoria zipo kanda nane mbili zikiwa Kenya.
Mshiu alisema nchini kanda maarufu ya
dhahabu ni Sukuma Land ambayo inahusu
Buzwagi, Bulyanhulu na Geita.
Dk Mshiu alisema hoja ya Serikali kutaka
mtambo wa kujengwa nchini ni lazima wataalamu washirikishwe ili kuuhakikishia
umma kuwa makinikia yatakuwapo ya kutosha.
Kuhusu kontena za tani 20 bandarini kuwa
na dhahabu asilimia 90 alisema ni kitu ambacho hakiwezekani kwani kwa uzito wa
dhahabu hiyo magari yasingetembea.
“Yote yanayofanywa yanafaa kupewa nafasi
ila kiuhalisia haiwezekani kontena la tani 20 likawa na asilimia 90 kwa uzito
wa dhahabu gari haliwezi kutembea,” alisema.
Kamati iliyoundwa na Rais inaongozwa na
Profesa Abdulkarim Mruma na wengine ni Profesa Justinian Rwezaura, Profesa Joseph Buchweishaija, Dk Yusuf Ngenya,
Dk Joseph Yoweza, Dk Ambrose Itika, Mohamed Makongoro na Hery Gombela.
Aidha, Bunge kupitia Spika Job Ndugai litaunda
tume ya kibunge kuchunguza sakata hilo la mchanga wa dhahabu.
0 comments:
Post a Comment