Suleiman Msuya
Mwigulu Nchemba |
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mwigulu Nchemba, ameonya waumini wa dini nchini kuacha kutumia mwavuli wa dini kufanya
vitendo vya uhalifu ikiwamo kudhuru maisha ya wengine, huku akitangaza kulegeza
masharti ya usajili wa nyumba za ibada.
Mwigulu alitoa onyo hilo juzi kwenye Tamasha
la Pasaka lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, akisema Serikali
haitavumilia watu wa aina hiyo.
Alisema Serikali inatambua uhuru wa
kuabudu iliyoutoa kwa wananchi wake na inaunga mkono kazi nzuri inayofanyika
kupitia ibada, lakini uhuru huo usikwaze wengine wala usivunje sheria.
"Ucha Mungu si udini", hivyo
ni sahihi kwa waumini kumcha Mungu kwa kiwango wanachopenda, lakini si
kuwashikia silaha watu wengine ili wajiunge na dini zao.
“Wale ambao watatumia misimamo
iliyopitiliza kudhuru maisha ya watu wengine, Serikali itasimama na kuwahesabia
kuwa ni waovu na tutashughulika nao kama wahalifu wengine,” alionya.
Nchemba aliagiza taasisi zilizo chini ya
wizara yake, kulegeza masharti ya usajili wa nyumba za ibada, badala ya kuwapa
njia ngumu kwani nyumba hizo ni muhimu kwa ajili ya kuombea viongozi na Taifa.
"Elekezeni watu wanaotaka kusajili
nyumba za ibada watimize masharti na muwasajili, hatuwezi kuweka masharti
magumu ya kusajili nyumba za ibada halafu tukaweka masharti rahisi ya kusajili
baa na kumbi za disko," alisisitiza.
Pia alitumia nafasi hiyo kuhakikishia
wasanii wa nyimbo za Injili kuwa Serikali itafanya kila iwezalo kulinda maslahi
ya kazi zao, huku akipongeza kazi nzuri inayofanywa.
0 comments:
Post a Comment