Pia walizungumzia harufu ya ufisadi
unaotaka kulikumba Taifa katika taasisi mbalimbali, uliooneshwa kwenye ripoti
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na suala la mishahara
hewa na vyeti bandia.
Katika mahubiri yao, maaskofu hao walieleza
kuwa matendo hayo maovu hayafanywi na Wapagani pekee, bali hata wenye dini
wakiwamo Wakristo, hivyo jamii inapaswa kuungana katika kuliombea Taifa wakati
wa tafakuri hii ya kufufuka kwa Yesu Kristo.
Wakasema Pasaka inaadhimishwa kwa
ufufuko, hivyo mwanadamu anapaswa kumkataa shetani na fahari zake zote, lakini
wengi wamekuwa wakienda kinyume.
Maaskofu hao walifafanua kuwa endapo
matendo ya mwanadamu yatakuwa ya giza, ina maana mtu huyo amekuwa mmisionari wa
shetani na si Mungu, kwani Mungu anapendezwa na yaliyo mema.
Kauli za maaskofu hao zimekuja huku
kukiwa na mjadala ulioibuka bungeni, kuhusu nani anahusika katika utekaji wa
msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ibrahim Musa ‘Roma Mkatoliki’ na Ben Saanane,
aliyekuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Sisi tunaamini kuwa kauli hii ya
viongozi wa dini imekuja wakati mwafaka, kwani mambo hayo yote ya utekaji,
mauaji ya polisi, vyeti bandia na mishahara hewa, hayajapatiwa ufumbuzi wa
kudumu.
Hivyo tunatoa mwito kwa jamii kutendea
kazi kauli hiyo ya maaskofu tukiamini kuwa kila mwanajamii ana nafasi sawa
katika kuyatafutia ufumbuzi masuala haya.
Tunaamini kuwa wakati Serikali na vyombo
vyake vya Dola vikiwa na jukumu la kuendelea kuwatafuta walioteka raia hao na
kusaka walioua polisi mkoani Pwani, jamii ina wajibu wa kutambua wahalifu hao
na kutoa ushirikiano wa ushahidi kama utahitajika.
Mchango wa jamii katika kusaka wahalifu
upo katika ukweli wa hao wanaoitwa majambazi. Pia hao wanaoendelea kujineemesha
kwa vyeti bandia wanafahamika kwa majina yao halisi mitaani.
Tunaamini kuwa kama jamii itaunganisha
nguvu na ikafanya kazi kwa karibu na vyombo vya Dola katika kukabiliana na
suala hilo, watu hao wasiolitakia mema Taifa letu watabainika na kuchukuliwa
hatua kali za kisheria.
Ifahamike, kwamba viongozi wa dini si
watendaji, ila ni wawakilishi wa Mungu duniani, hivyo tuchukue mwito wao kama mwito
kutoka kwa Mungu na tuufanyie kazi, linalowezekana leo lisingoje kesho. Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki
Tanzania.
0 comments:
Post a Comment