Abraham Ntambara
Januari Makamba |
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Januari Makamba, amesema hali ya mazingira nchini si nzuri kutokana na
ulegevu wa muda mrefu wa kusimamia sheria za uhifadhi.
Makamba
alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam baada ya ufunguzi wa mkutano wa siku tatu
ulioandaliwa na Korea kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) ambao
utazungumzia maendeleo endelevu kwa kutumia teknolojia inayozingatia hifadhi ya
mazingira.
“Hali
si nzuri kusema ukweli, kumekuwa na ulegevu wa muda mrefu katika kusimamia
sheria ya uhifadhi wa mazingira, sasa hivi kidogo tunaamka na kuongeza kasi na
ukali zaidi ili kulinda mazingira,” alisema Makamba.
Alisema
hayo yanafanyika ili kuhakikisha mito na vyanzo vya maji haviharibiwi, misitu
inahifadhiwa na viwanda havimwagi sumu na kutoa moshi ambapo alieleza kuwa kwa
sasa pia watu wanafanya tathmini ya athari kwa mazingira kutokana na shughuli
zao za uchumi.
Alisema
kuelekea ujenzi wa viwanda ni vema kuweka hali ya mazingira vizuri hivi sasa
ambapo kuna dhana miongoni mwa jamii kuwa tujenge kwanza na suala la mazingira
litashughulikiwa baadaye.
Aliongeza
kuwa anaamini mkakati wa ujenzi wa viwanda nchini utakwenda sambamba na
uhifadhi wa mazingira, kutokana na kwamba nchi zenye viwanda zimekuwa
zinaathiriwa na uchafuzi wa mazingira.
Makamba
alisema Korea ni nchi ya mfano inayoonesha kuwa pamoja na maendeleo ya viwanda,
uhifadhi wa mazingira pia unawezekana.
Mkutano
huo unajumuisha wataalamu, wasomi na wakuu wa taasisi duniani zinazoshughulika
na maendeleo na mazingira.
0 comments:
Post a Comment