*Asema yeye ni mmoja wa walio kwenye orodha
*Abainisha
kudokezwa na baadhi ya mawaziri
Sharifa Marira, Dodoma
Hussein Bashe |
WAKATI matukio ya uvamizi na watu maarufu
kutekwa yakiendelea kutikisa Taifa, Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe (CCM) amezua
takaruki bungeni baada ya kufichua kuwepo mpango wa yeye na wabunge wengine 10
kutekwa.
Amesema taarifa hizo amepewa na baadhi
ya mawaziri, wakimhadharisha kuwa makini, kwa maelezo kwamba yeye na wenzake
wanaweza hata kupoteza maisha kwa sababu tayari wameingizwa kwenye orodha.
Mbunge huyo kijana anayesifika kwa tabia
yake ya kuikosoa Serikali, bila woga alitoa kauli hiyo jana baada ya kuomba
Mwongozo wa Kiti cha Spika, akitaka kikao cha jana cha Bunge la Bajeti kiahirishwe
ili kujadili matukio ya utekaji nchini.
Katika maelezo yake huku akitumia Kanuni
ya 47 ya Bunge, Bashe alisema: “Zipo taarifa binafsi nimezipokea kutoka kwa baadhi ya
mawaziri wakinihadharisha.
“Wamenitaka
niwe makini, kwa sababu ni miongoni mwa wabunge 11 ambao wamewekwa katika orodha.
Nimeelezwa nikikaa barabarani vibaya tunaweza hata kupoteza maisha.”
Aliongeza:
“Kikundi hiki (cha utekaji) kilicho ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa ambacho
kimeamua kuchukua mamlaka haya ya kuteka watu, kinaharibu heshima ya Serikali
yetu na chama changu ambacho mimi na wabunge wenzangu tuliomba ridhaa ya kuongoza
Watanzania na si kuwahatarishia maisha.”
Hata hivyo, Mwongozo alioomba mbunge
huyo uliofanana na wa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbililinyi ‘Mr Sugu’
(Chadema), ulipingwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kwa maelezo kuwa si jambo
la dharura na litatatuliwa na mamlaka zilizopo.
Bashe alitoa kauli hiyo kukiwa na
kumbukumbu ya kupotea kwa Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema, Ben
Saanane tangu Agosti 8 mwaka jana na tukio la siku nne zilizopita, la kutekwa
na kuachwa kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Musa Ibrahim ‘Roma Mkatoliki’
na wenzake wanne.
Wakati Bashe akieleza kuwapo Watanzania
wengi wanaotekwa lakini kwa kuwa si maarufu, utekaji wao haujulikani, Mbilinyi
alimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kujiuzulu kwa
kushindwa kudhibiti matukio hayo.
Ilivyokuwa
Baada ya kipindi cha maswali na majibu
jana asubuhi, wabunge wengi walisimama kwa nia ya kuomba Mwongozo, ndipo Dk
Tulia alipompa nafasi Bashe.
Katika
Mwongozo wake, Mbunge huyo alieleza kuwa matukio ya utekaji yamekuwa yakitokea
mfululizo bila hatua stahiki kuchukuliwa.
“Kumekuwa
na matukio ya sintofahamu nchini, si tu kwa wabunge ila hata raia. Kuna kikundi
kinateka watu na miongoni mwa waliowahi kutekwa ni Msukuma (Joseph -Mbunge wa
Geita Mjini-CCM), mimi mwenyewe na Malima (Adam-aliyekuwa Mbunge wa
Mkuranga-CCM) wakati wa mkutano mkuu wa CCM,” alisema Bashe.
Huku
akihoji kupotea kwa Saanane ambaye alikuwa msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe na Roma, alisema hao ni wanaojulikana, lakini wapo Watanzania
wengine wanaotekwa.
Katika
Mwongozo wake, Bashe aliomba Kiti cha Spika kuridhia kujadili jambo hilo na
kuunda kamati maalumu ya kuchunguza utekaji na ikishindikana jukumu hilo
lipelekwe kwa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, kufanya
uchunguzi na kutoa taarifa kwa ajili ya usalama wa wananchi.
“Hali
ya nchi si salama, Watanzania wana taharuki na wanajadili mambo haya katika
mitandao ya kijamii kila kukicha, lakini hakuna kauli ya matumaini kutoka
serikalini. Waziri wa Mambo ya Ndani yuko wapi?’’ Alihoji Bashe.
Mbilinyi
katika Mwongozo wake, alisema Taifa ni kama liko gizani kutokana na utaratibu
mpya uliozuka kwa kuteka watu aliodai kuwa ni mpya nchini.
“Utamaduni
huu kwa mara ya mwisho ulitokea Zanzibar alipotekwa Kassim Hanga, lakini tangu
operesheni hii ya kukamata watu ianze, kila anayehusika na usalama wa nchi,
likiwamo Jeshi la Polisi wakiulizwa wanasema hawana taarifa,” alisema Mbilinyi
akiongeza:
“Amepotea
Saanane, Roma na wengine, kuna miili ya watu iliokotwa Mto Ruvu lakini viongozi
wako kimya.”
Huku
akimtaka Mwigulu kujiuzulu kama anaona hashirikishwi katika mambo yanayoendelea
nchini, Mbilinyi alisema haiwezekani Waziri kukaa kimya na kutoa tafsiri kuwa
amefumbwa midomo.
“Najiuliza
kama anabanwa kwa kiasi hicho huyu ni mtu potential (mwenye uwezo) aligombea
hata urais, ana miaka mingi ya kuwa kiongozi. Kwa nini asijiuzulu alinde heshima
yake kuliko kukaa kimya?” Alihoji.
Mbilinyi
alisema hata Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi akiwa Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, alijiuzulu, lakini baadaye akawa Rais.
Alisema
Roma alipatikana siku chache baada ya kiongozi mmoja wa Serikali ya Mkoa wa Dar
es Salaam kutamka wazi kuwa msanii huyo atapatikana kabla ya Jumapili ya Aprili
4.
“Mtu
aliyesema anamrudisha Roma, tumlazimishe, maana tunajua anafahamu mambo haya,
hivyo atueleze aliko Saanane na ile miili sita ilikuwa ya watu gani,”
alisisitiza.
Licha
ya miongozo hiyo kuonekana kuliteka Bunge, Dk Tulia alisema kwa mujibu wa
kanuni ya 47 ambayo husomwa pamoja na ya 48, ili kuweka masharti ya
matumizi ya kanuni ya 48 (4), inaeleza jambo lolote litahesabiwa kuwa la
maslahi kwa umma, iwapo utatuzi wake utategemea hatua zaidi kuliko utekelezaji
wa kawaida wa sheria peke yake.
"Miongozo
iliyotolewa na Bashe na Mbilinyi itatatuliwa na taratibu za kawaida za sharia,
hivyo sihesabu kama jambo la dharura kama lilivyowasilishwa,” alisema.
0 comments:
Post a Comment