Mwandishi Wetu
Rais John Magufuli |
WAKATI watumishi wa umma 9,932 wakiondolewa
serikalini kwa kughushi vyeti huku wakinusurika kushitakiwa kwa jinai, Serikali
imekwepa kuchunguza vyeti vya wanasiasa, akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
anayetuhumiwa kughushi vyeti.
Akiwasilisha ripoti ya ukaguzi wa vyeti
vya watumishi hao mbele ya Rais John Magufuli jana katika ukumbi wa Chimwaga wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki alitaja viongozi
ambao vyeti vyao havikukaguliwa.
Kwa mujibu
wa Angellah,
ukaguzi huo uliobaini watumishi hao wakiwa na vyeti vya kughushi, haukuhusu
viongozi wa kisiasa wakiwemo mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya
wala madiwani.
Angellah alifafanua kuwa viongozi hao
hawakukaguliwa vyeti kwa kuwa sifa za uongozi wao ni kujua kusoma na kuandika.
Serikali imechukua hatua hiyo wakati
tayari mashitaka dhidi ya Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam, yakiwa katika Tume
ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoka kwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface
Jacob.
Katika mashitaka hayo, Jacob anamtuhumu
Mkuu huyo wa Mkoa kwa kughushi vyeti vya kitaaluma huku akijua fika kuwa vyeti
anavyotumia si vyake.
Jacob amedai katika mashitaka hayo kuwa
Mkuu huyo wa Mkoa, amekiuka sheria za nchi kwa kula kiapo cha utii na uaminifu
mbele ya Rais kwa uhusika wa kughushi.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti
hiyo, Rais Magufuli mbali na kutaka watumishi waliokutwa na vyeti vya kughushi
kuondoka wenyewe kabla ya Mei 15, alizungumzia tatizo lingine la wafanyakazi
hewa serikalini.
Alisema alipoingia madarakani, walifanya
ukaguzi na kukuta watumishi hewa 19,706 na kuhoji hivi hakukuwa na mawaziri? Hakukuwapo
makatibu wakuu na viongozi wengine?
“Tulijiuliza kwa nini tunalipa fedha nyingi
za mishahara zaidi ya Sh bilioni 700 kila mwezi, posho, likizo, michango kwenye
mifuko ya jamii, tukachukua hatua, hebu tujaribu kutafuta kweli hawa watumishi
wapo?” Alisema.
Alisema uchunguzi ulifanyika na kubaini
watumishi 19,706 hivyo kwa sasa linaendelea.
Rais Magufuli alisema wanapozungumzia
watumishi hewa 19,706, walikuwa wakichukua Sh bilioni 19,848 kila mwezi za
mshahara hivyo ilisababisha hasara ya Sh bilioni 238.2 kwa Serikali kwa mwaka.
“Tumewatoa wote hawa watumishi hewa,
lakini najua bado wapo kama asilimia moja au mbili wale nao endeleeni
kuwachambua vizuri,” alisema.
Aliongeza kuwa baada ya kuondoa watumishi
hao, mishahara kwa mwezi na matumizi yalipungua kutokana na vitu hewa vyote
kuondolewa.
“Tulijiuliza sana kama tumepata
watumishi hao hewa tulikuwa tunapandisha vyeo hewa, hivyo tukaona twende kwenye
kazi ngumu ambayo nchi nyingi zimeshindwa kuitelekeza ya kuchambua wenye vyeti
hewa,” alisema na kuongeza:
“Unakuta mtu ana cheti kumbe ni cha
mdogo wake au marehemu, unakuta anakitumia, wakati kuna watu wanahangaika
kutafuta ajira na wana vyeti vilivyokamilika kama hapa, kumbe serikalini yapo
majamaa hayana hata vyeti.”
Rais Magufuli alisema ndiyo maana
michakato hii yote inafanyika na anajua kuwa lazima kuna watu watachukia, kwa sababu
ya kuwaondoa ambao wameghushi vyeti.
Alisema walioondoka watamchukia lakini
hawana cha kufanya, maana ndio wameondoka na anajua wataendelea kumchukia,
lakini ambao watapata nafasi hizo na wana sifa watamwombea.
0 comments:
Post a Comment