*Awapa mpaka Mei 15 kuondoka wenyewe serikalini
*Aagiza
watakaobaki wakamatwe wafungwe miaka 7
Mwandishi Wetu
Rais John Magufuli |
RAIS John Magufuli amesamehe kuwafikishwa
mahakamani na kuwafunga miaka saba jela kwa watumishi 9,932, walioghushi vyeti,
ikiwa wataacha kazi kabla ya Mei 15.
Alitoa kauli hiyo Dodoma jana wakati
akipokea taarifa ya uhakiki wa vyeti bandia vya watumishi wa umma, akisema
suala hilo kwa kiasi kikubwa limesababisha utendaji kazi mbovu, huku akionesha
kushangazwa na viongozi waliopita kuacha suala hilo liendelee.
“Hatuwezi kuwa na Taifa la watu wasio na
sifa, nafasi zitangazwe ili watu waombe … wanajijua, hivyo bora waondoke na
watangazwe kwenye magazeti maana hao ni majambazi na mijizi kama mingine,” alisema.
Aliagiza pia kuwa watu hao 9,932
mishahara yao ikatwe na waondoke mara moja na watakaobaki baada ya Mei 15,
vyombo vya ulinzi na usalama viwakamate na kuwafikisha mahakamani, ili wafungwe
miaka saba kwa mujibu wa sheria.
Rais Magufuli alisema Tanzania haijasema
inaajiri watu wenye Shahada, bali kuajiriwa kwake kunatokana na kiwango cha elimu
alichonacho mwomba ajira, hivyo kuwataka waliofukuzwa kutafuta kazi
zinazoendana na viwango vya elimu walivyosomea.
“Kila mtu aende panapomfaa, lakini kama
mtu ameshindwa kufika sehemu anayotaka asiruke kwa kupita njia za mkato, bali
ajiendeleze na si kudanganya, kwa kuwa ni kosa kubwa na adhabu ni kubwa,” alisema
na kuongeza:
“Watakaojiondoa msiwapeleke mahakamani
na hadi Mei 15 ambao watakuwa hawajaondoka wenyewe, polisi kamateni, wapelekeni
wakajibu walipata wapi vyeti hivyo.”
Wanaoshirikiana vyeti
Kuhusu watumishi 1,538, ambao vyeti vyao
vimekutwa vikitumiwa na watu zaidi ya mmoja, Rais Magufuli aliagiza wasilipwe
mshahara wa mwezi huu, hadi wenye vyeti halali watakapojitokeza.
Alisema huenda idadi ya watumishi wasio
na vyeti vinavyoendana na nafasi zao wakafikia 12,000 na kuagiza ajira zao
zitangazwe na kupewa wanafunzi wanaomaliza vyuo na wanaohangaika kutafuta kazi,
wakati wana sifa.
Ripoti
Awali wakati akisoma ripoti hiyo kabla
ya kuikabidhi kwa Rais Magufuli, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alifafanua kuwa kazi hiyo haikuwa rahisi, kwa kuwa walikuwa
wanabezwa na watu kuwa kama sensa inaweza kuchukua hata siku mbili, kwa nini
suala la vyeti limechukua muda.
Alisema taarifa hiyo iligawanywa kwenye
makundi manne; la kwanza lilihusisha wenye vyeti halali 376,969 sawa na
asilimia 94.2 ambavyo vilionesha magamba yao yalitolewa na Baraza la Taifa la
Mitihani (Necta) na taarifa zao zinafanana na zilizo kwenye kanzidata ya Baraza
hilo.
Alisema kundi la pili lilihusisha watu
walioghushi ambao ni 9,932 sawa na asilimia 2.4 ambapo vyeti vyao vilikuwa na
magamba, alama za siri na muundo ambao haufanani
na vya Necta na baadhi taarifa zao zilifutwa na kuandikwa upya tofauti na
zilizo kwenye kanzidata.
Kundi la tatu lilikuwa la vyeti
vilivyotumiwa na mtu zaidi ya mmoja, ambao walikuwa 1,538 sawa na asilimia 0.3 huku
watumishi wa umma 376 wakionekana kutumia cheti kimoja zaidi ya watu wawili
hadi watatu.
“Kila jina la cheti linafanana na lililo
kwenye kanzidata, wengine unakuta halijafanana kwa kuwa majina yanakuwa
yameongezwa mwishoni, mwanzoni au limewekwa kifupi katikati na taarifa zao
zinatofautiana na zilizo kwenye kanzidata,” alisema.
Kundi la nne ni vyeti vyenye upungufu,
ambapo watumishi 11,596 walibainika kuwasilisha vyeti vya taaluma pekee na
hawakuweka cha kidato cha nne wala sita.
Alisema hilo ndilo eneo pekee linalowapa
shaka na wanajiuliza kama mtu huyo alipataje cheti cha taaluma na kuwataka
waajiriwa hao kupeleka vyeti vya kidato cha nne au cha sita kwa waajiriwa wao.
Viongozi
Kabla ya taarifa hiyo na kabla ya Rais
Magufuli kuzungumza, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alitaka wanafunzi wa
Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), kilichokuwa kikitimiza miaka 10 jana, kusoma kwa bidii
kwa kuwa ndio wanaotazamiwa kuongoza nchi kwa miaka ijayo watakapoachiwa na
viongozi wanaopita.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana
alimpongeza Rais kwa kufanyia mkutano wake chuoni hapo ikiwa ni mara
ya kwanza kwa kuwa waliitamani sana nafasi hiyo.
“Naomba nikiri kuwa tulikuwa tunapata
wivu ulipokuwa unakwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) tukawa tunajiuliza
utakuja huku lini, hivyo mmekuja wote tumefurahi sana,” alisema na kuongeza.
Mimi ni msaidizi wako hapa Dodoma,
nawafahamu wanafunzi wako vizuri anayesema wana matatizo ni majungu, wako ‘bomba’
wanatoa ushirikiano wameweka utaratibu mzuri, ndiyo maana hatujawahi kuzungumza
chochote kuhusu hawa wananfunzi.
Aliongeza kuwa mkoa wake umeweka
utaratibu wa kushirikiana na wanachuo, wanaohusika na afya, walimu barabara,
hivyo wameweka utaratibu kuhakikisha
wanawasaidia ili wasisumbue kwenye ‘Boom (posho za mwezi)’.
Mkuu UDOM
Makamu Mkuu wa UDOM, Profesa Idris
Kikula alisema hatua ya Rais kwenda chuoni hapo inaonesha namna anavyokijali
licha ya kuwa na mambo mengi ya kufanya.
Alisema chuo hicho kinatimia miaka 10
tangu kilipoanzishwa kwa kudahili wanafunzi zaidi ya 40,000, hadi sasa kina
vyuo saba na wanafunzi 23,163 ambapo wengine wanasomea shahada za awali wengine
za juu.
“Kimesomesha wafanyakazi zaidi ya 400
kwa kutumia vyanzo vyake vya ndani vya mapato na kupunguza idadi ya wanataaluma
na gharaa kwa Serikali pamoja na kutoa ajira,” alisema.
Alisema mashine 10 zilipatikana kutoka
kwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa ambazo zimeokoa wagonjwa wa figo zaidi ya 400
huku zaidi ya watu 500 wakipata huduma ya Ukimwi.
Aliongeza kuwa changamoto zilizokuwa
zinasumbua ni uhaba wa walimu na maji, hali iliyosababisha wakapunguza kasi ya
udahili ili kukabiliana nayo na kwa sasa mitambo imeshajengwa, hivyo udahili
unaendelea kama kawaida.
Aidha, maandalizi ya kupandikiza figo kwenye
hospitali ya Benjamin Mkapa yako tayari na wataalamu watakwenda Japan kujifunza
wakirudi watafanya kazi hiyo.
Profesa Kikula alisema chuo pia kimeajiri
na kusomesha wataalamu wa kuchunguza uhalifu unaotendeka kupitia mitandao.
0 comments:
Post a Comment