Celina Mathew
Maalim Seif Sharif Hamadi |
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemtaka Maalim Seif Sharif
Hamad kueleza ukweli ili jamii ipate kuelewa kinachoendelea ndani ya
chama hicho hasa kuhusu mambo muhimu.
Hayo ni pamoja na suala la nafasi yake ya ukatibu mkuu kukaimiwa,
Bodi ya Wadhamini na kesi nne mahakamani, ambazo Seif na wenzake walifungua.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa CUF,
Magdalena Sakaya jana ilieleza kwamba anachofanya Maalim Seif na wenzake ni
kuwatoa wana CUF kwenye hoja za kikatiba za kushughulikia mgogoro wa uongozi
ndani ya chama hicho.
Kuhusu suala la kukaimiwa kwa nafasi ya Katibu Mkuu,
Sakaya alisema hilo ni suala la kikatiba
na si utashi wake au wafuasi wake.
"Tumeeleza na kunukuu ibara ya 93 kifungu cha 2 mara
kadhaa. Kifungu hiki kinampa madaraka Naibu Katibu Mkuu anayetoka upande wa
pili wa Muungano tofauti na anaotoka Katibu Mkuu, kukaimu nafasi na kutekeleza
majukumu ya Katibu Mkuu mpaka pale Katibu Mkuu atakapokuwa tayari kutekeleza
majukumu yake," ilisema taarifa hiyo ikimnukuu Sakaya.
Alisema anachopaswa kufanya Maalim Seif ni kusema kifungu
hicho hakipo au hakisemi hivyo, ili jamii ipate kuelewa na si kubadilisha
maneno.
“Ni kweli CUF tumeandika barua kumjulisha Msajili wa
Vyama vya Siasa kuhusu suala hilo naye amejibu akikiri kupokea barua na
ameridhia kwa mujibu wa Katiba yetu,” alisema.
Alisema Profesa Lipumba na Maalim Seif hakuna kati yao
mwenye uwezo wa kumsimamisha mwenziwe au kuteua mtu wa kukaimu nafasi ya
mwenziwe na kwamba suala la Maalim Seif kuomba kusajili Bodi mpya, na nakala ya
maombi hayo kuyawasilisha Ofisi ya Msajili ni kichekesho kama si kujichanganya.
"Maalim Seif na genge lake wamefungua kesi Mahakama
Kuu ya kutotambua msimamo na ushauri wa Msajili kuhusu uliokuwa mgogoro wa
uongozi ndani ya CUF na inaitaka Mahakama Kuu itamke kuwa Msajili wa Vyama hana
haki ya kuangalia mambo ya ndani ya CUF.
“Swali kwa Maalim Seif na genge lake, je
wanapopeleka nakala ya maombi ya kusajiliwa Bodi yao Ofisi ya Msajili huko si
kuingilia mambo ya ndani ya vikao vya chama ? Au ndio kusema kwamba sasa Seif
na genge lake wameamua kumtambua Msajili kupitia nyuma ya pazia?”
Aliongeza kuwa lingekuwa jambo jema kama Maalim Seif sasa
angekiri wazi kwamba chama hicho kikatiba hakina Bodi halali kama ambavyo Msajili
alisema kwamba Bodi ya Wadhamini ya CUF ni mfu na haipo kisheria, ndiyo maana
sasa anahangaika kusajili Bodi mpya.
Alihoji kama hivyo ndivyo, je Maalim Seif anaweza
kuieleza jamii na wana CUF kwa ujumla kuwa zile kesi nne mahakamani zilifunguliwa
na Bodi ipi ikiwa hivi sasa yeye anaomba kusajili Bodi mpya? Au ndiyo kusema
ameamua kufuta kesi zote kimyakimya?
Aliongeza kuwa ni vema akasema wazi ikiwa maombi yake ya
kufungua Bodi mpya yatakubalika na kueleza ni ipi sasa itasimamia kesi mahakamani.
"Maalim Seif hajui atendalo kwa sasa, ni vyema
amwache Kaimu Katibu Mkuu Sakaya na Kamati mpya ya Utendaji wasimamie
shughuli za chama ikiwamo ya kuwafanyia kampeni na kuwaombea kura wagombea wetu
wa Bunge la Afrika Mashariki na Kaimu Katibu Mkuu yuko Dodoma akifanya
kampeni kwa wagombea wetu Habib Mnyaa, Thomas Malima na Sonia Magogo,”
alisisitiza.
Aliwajulisha wana CUF kokote waliko na Watanzania kwa jumla
yao kuwa chama hicho kiko katika mikono salama ya viongozi wanaojitambua ambao
hawaendeshwi kwa fedha za kifisadi, bali wanaendesha chama kwa mujibu wa Katiba
yake ya mwaka 1992 toleo la 2014.
0 comments:
Post a Comment