*Asema anazeeka kuliko JK kwa kazi ngumu
*Atakayejaribu
kuvunja Muungano atavunjika
Celina Mathew
Rais John Magufuli |
RAIS John Magufuli amesema anaonekana
mzee kuliko Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kwa sababu kuongoza nchi ni kazi ngumu
akieleza kuwa ana kazi kubwa kuulinda Muungano na kuonya mtu atakayejaribu kuuvunja
kuwa atavunjika yeye.
Alisema hayo jana alipohutubia wananchi kwenye
maadhimisho ya Miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kitaifa
kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Mji huo ambao ndio makao makuu ya
Serikali jana ulipambwa na shamrashamra za siku hiyo, iliyojumuisha maelfu ya
wakazi na wageni wa kitaifa na kimataifa kwenye uwanja huo, ambapo pamoja na mambo
mengine ulipambwa na maonesho ya ndegevita.
Huku akitoa mfano wa waasisi wa Muungano
na marais wa awamu zilizomtangulia, katika hotuba yake iliyojaa utulivu, Rais
Magufuli alitumia nafasi hiyo kuelezea namna viongozi hao walivyolinda Muungano.
“Kuongoza ni kazi ngumu, mimi nazeeka kutokana
na majukumu na kazi niliyonayo, lakini mnamwona Rais mstaafu, Mzee Jakaya
Kikwete anaonekana bado kijana kuliko mimi,” alisema.
Aliongeza: “Mimi na Rais wa Zanzibar Dk Ali
Mohammed Shein tutalinda Muungano vizuri sana kama viongozi waliopita, kama
tulivyoapa kuulinda na akitokea mtu yeyote kujaribu kuuvunja atavunjika yeye.”
Akizungumzia umuhimu wa amani, Rais
Magufuli alisema bila tunu hiyo, hakuna kitakachowezekana nchini na kwamba ili
yote yafanikiwe, lazima Muungano ulindwe kwa kuhakikisha wanaenzi yaliyoachwa
na viongozi waliopita.
“Mimi na Shein tutafuata nyayo za
viongozi waliopita kulinda Muungano. Leo tunaposherehekea tutafakari
tulikotoka, tuliko na tunakokwenda,” alisisitiza.
Aliwataka Watanzania bila kujali
makabila wala itikadi zao, kuungana kuulinda Muungano ili jina Tanzania lidumu
na uweze kusherehekewa miaka mingi ijayo.
“Tulinde na kudumisha Muungano ili jina
la Tanzania lidumu, nafahamu tukishikamana kwa pamoja tutaweza na tutasherekea
miaka mingi ijayo,” alisema Rais Magufuli.
Mafanikio
Rais Magufuli alisema miaka 53 ya
Muungano imeshuhudia mafanikio makubwa na kujengwa kwa Taifa lenye nguvu.
Alisema hadi sasa Tanzania ni nchi ya
amani na mipaka yake ni salama, hali inayoifanya kufanya mambo kwa kujiamulia yenyewe.
“Tumepata mafanikio kwenye nyanja za
kiuchumi, kisiasa na kijamii, uchumi umekuzwa na kukabiliana na umasikini na
utegemezi hususan kwenye umeme, shule zimeongezeka, miradi ya maji imeboreshwa,
demokrasia imepanuka, hivyo Tanzania ya sasa si ya mwaka 1964,” alisema.
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni nchi kuheshimika
kikanda, kibara na duniani, pia kushiriki kutafuta na kulinda amani.
Alisema wapo waliofanya kazi kuhakikisha
mambo hayo yanafanikiwa kwa kuwa kuleta Muungano si jambo rahisi.
“Kuleta Muungano ni vigumu kwa kuwa hata
kulinda ndoa zetu imekuwa vigumu, hivyo kulinda Muungano si jambo rahisi,”
alisema akitania.
Alitaja baadhi ya waasisi waliosababisha
kuzaliwa na kudumu kwa Muungano kuwa ni Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius
Nyerere, marehemu Shekhe Abeid Amani Karume na viongozi wa awamu zote
zilizopita, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Kikwete.
“Leo katika kuadhimisha Muungano huo
hapa tuna Mama Maria Nyerere na Fatma Karume,
nawashukuru viongozi waliopita kwa kulinda Muungano hadi leo,” alisema.
Changamoto
Alisema licha ya mafanikio pia kuna
changamoto zilizosababisha kuundwa kamati ya pamoja ambayo Mwenyekiti wake ni
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Seif Iddi
na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Alisema viongozi hao wanafanya kazi
vizuri huku akisisitiza Watanzania kuhakikisha wanashirikiana nao na si
kuwaacha peke yao kwa kuwa suala la Muungano ni la kila mtu huku akiwataka kuchapa
kazi kwa bidii.
Dodoma
Rais Magufuli alisema kwa mara ya kwanza
sherehe hizo zimefanyika makao makuu ya Serikali, hivyo ni ishara kuwa
imedhamiria kuhakikisha yanakuwa kule.
Alisema katika kuhakikisha hilo
linatimia, awamu hii ya kwanza tayari watumishi 3,000 wamehamia Dodoma na wengine
wanaendelea.
Aliongeza kwa mwaka ujao wa fedha
zimetengwa Sh bilioni 200 kwa ajili ya mchakato huo wa kuhamia kwa wafanyakazi
waliobaki kwa awamu ya pili na tatu.
Aidha, alisema kuna mambo yanaendelea
kufanyika ikiwa ni pamoja na ujenzi wa treni ya umeme kutoka Dar es Salaam-
Dodoma, maboresho na ujenzi wa barabara, uwanja wa mpira na miundombinu ya maji.
“Tunafanya hivyo ili kuhakikisha
tunajenga miundombinu mizuri kwa wananchi wa Dodoma na Serikali kwa ujumla. Leo
tunaona wananchi wamejitokeza kwa wingi hii inadhihirisha Dodoma ni makao makuu
ya nchi,”alisema.
Awali, Rais Magufuli alisema siku ya
jana ilikuwa siku ya historia kwa Taifa, hivyo kila Mtanzania ajivunie kwa kuwa
ni Siku ya Kuzaliwa Tanzania.
Alisema mwaka 1964 Taifa jipya
lilizaliwa baada ya Karume na Nyerere kusaini na kuchanganya udongo wa nchi
hizo mbili (Tanzania na Zanzibar) na hivyo kuleta Muungano.
Alisema huo ni udugu wa kihistoria ulio kwenye
kushirikiana na mataifa mbalimbali katika masuala ya kibiashara na uhusiano mzuri
ulioletwa na TANU na Afro Shiraz, ambavyo viliunganisha nchi hizi mbili.
Wakati akimkaribisha Rais Magufuli
kuzungumza na Watanzania, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema
kilichoshuhudiwa jana ni tendo la kwanza la kihitoria kwa mkoa wake na kwamba
ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Maadhimisho hayo yalifanyika mkoani humo
kwa mara ya kwanza katika historia ambapo maadhimisho hayo yalipambwa na
gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama vilivyopita mbele ya Rais kutoa
heshima, vikundi vya burudani ikiwamo muziki, halaiki, kwaya na ngoma za
kiasili.
0 comments:
Post a Comment