*Polisi wanane, watuhumiwa ujambazi wanne wauawa
*Majambazi waonywa hakuna
atakayenusurika
Mwandishi Wetu
MAUAJI yaliyotokea eneo la Jaribu
Mpakani, wilaya ya Kibiti mkoani Pwani yamefikia watu 12, kati yao askari
Polisi wanane na watuhumiwa wa ujambazi wanne.
Taarifa iliyotolewa jana na Kamishna wa
Jeshi la Polisi, Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya, ilieleza kuwa
watuhumiwa hao wa ujambazi waliuawa katika majibizano ya bunduki kati ya polisi
na majambazi.
Kwa mujibu wa Mssanzya, askari waliouawa
ni Inspecta Peter Kigugu; F.3451 CPL Francis;
F.6990 PC Haruna; G.3247 PC Jackson; H.1872 PC Zacharia; H.5503 PC Siwale; H.7629 PC Maswi na H.7680 PC Ayoub.
Mauaji ya askari 8
Kamisha Mssanzya alisema kuwa mauaji ya askari hao yalifanyika juzi 12:15 jioni
katika eneo la Mkengeni kijiji cha Uchembe kata ya Mjawa tarafa na wilaya ya
Kibiti mkoani Pwani.
Alisema kundi
la majambazi ambalo idadi yao bado haijafahamika wakiwa na silaha,
walishambulia kwa risasi gari la Polisi aina ya Toyota Land Cruiser PT.3713 na
kuua askari wanane.
Mbali na kuua
askari hao, pia walimjeruhi askari namba F. 6456 PC Fredrick kwa kumpiga risasi
ya mkono wa kushoto ambaye alipelekwa hospitali ya misheni Mchukwi kwa matibabu.
Yalivyofanyika
Taarifa
zinaonesha kuwa kundi hilo la majambazi wakiwa na silaha walishambulia kwa risasi gari hilo la polisi na kuuwa askari wanane papo hapo.
Ilielezwa kuwa
kabla ya kutokea mauaji hayo, gari hilo lilikuwa likitokea eneo la Jaribu Mpakani
kwenye kizuizi cha barabara kwenda Bungu likiwa na askari hao walikuwa wametoka
kubadilishana lindo.
Kwa mujibu wa
taarifa hizo, gari hilo lilipofika maeneo ya Mkengeni sehemu yenye mteremko na
majani marefu, lilianza kushambuliwa na majambazi hao.
Ilielezwa kuwa
majambazi hao walipiga risasi kwenye kioo cha mbele usawa wa dereva, hali
iliyomsababishia dereva kupoteza uelekeo na gari kuingia kwenye mtaro wa
barabara, ndipo majambazi hao wakafanya mauaji kwa askari hao.
Mauaji ya
watuhumiwa 4
Kamisha Mssanzya katika taarifa yake
alisema hatua za kiintelijensia na kiupelelezi zilichukuliwa juzi hiyo hiyo
usiku na zikasaidia askari kufuatilia na kubaini maficho ya muda ya majambazi
hao.
Taarifa hiyo ya Kamisha Mssanzya,
ilieleza kuwa katika majibizano ya risasi kati ya askari Polisi na majambazi
hao, ndipo watuhumiwa hao wanne waliuawa.
Hata hivyo, taarifa zingine kutoka
vyanzo vyetu zilidai kuwa baada ya mauaji ya askari hao wanane, Polisi ilifanya
mahojiano na watuhumiwa wa ujambazi waliokuwa
wakishikiliwa mahabusu.
Mahojiano hayo
kwa mujibu wa taarifa hizo, yalisaidia watuhumiwa kukubali kwenda kuonyesha
eneo walikojificha wenzao, katika msitu wa kilima cha Mianzini, barabara ya
Nyamisati kwenye majira ya nane usiku wa kuamkia jana.
Inadaiwa kuwa
walipofika eneo hilo, watuhumiwa hao waliokuwa mbele kwenda kuonesha waliko
wenzao, walishambuliwa na majambazi hayo kujeruhiwa na baadaye walikufa ndipo
majibizano ya risasi yakaendelea baina yao na polisi.
Bunduki
zilizopotea
Taarifa ambazo hazijathibitishwa Polisi, zilidai kuwa
baada ya mauaji ya askari hao, majambazi hao walikimbia na silaha tisa kati ya
hizo, SMG sita zikiwa na risasi 30 kila moja na Long range tatu.
Lakini taarifa ya Kamisha Mssanzya
ilieleza kuwa baada ya majibizano ya risasi wakati watuhumiwa wanne wa ujambazi
walipouawa, majambazi hao walitelekeza silaha nne; mbili zikiwa zilizoibwa
wakati wa mauaji wa askari na mbili mali ya majambazi hao.
Msako wa moto
Akielezea kwa
undani, Kamishna Mssanzya alisema tukio hilo ni baya na
halikubaliki kwani hadi sasa Jeshi la Polisi limeshapoteza askari zaidi 10
katika matukio kama hayo.
Alisema wameshaanzisha operesheni
maalumu ya moto na kutangaza kuwa hakutakuwa na msamaha, kwamba watatafutwa na
kushughulikiwa na hakuna atakayenusurika.
Kamishna Mssanzya alisema mapambvano hayo hayana mwisho na kuonya kuwa katika
operesheni hiyo, majambazi wataona sura halisi ya Jeshi la Polisi kwa kuwa dawa
ya moto ni moto.
Alimaliza kwa kupiga marufuku pikipiki
za biashara maarufu bodaboda kufanya kazi zaidi ya saa 12 jioni katika eneo
lote la Mkuranga, Kibiti na Rufiji.
JPM aomboleza
Wakati huo huo, Rais John Magufuli jana
alielezea kupokea kwa mshituko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya hao.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya
Rais, Ikulu Gerson Msigwa, ilieleza kuwa
Rais Magufuli alimtumia salamu za
rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP-Ernest Mangu, familia za askari
wote waliouawa, Askari Polisi wote na Watanzania wote walioguswa na vifo hivyo.
“Nimeshtushwa na nimesikitishwa sana na
vifo vya askari wetu wanane ambao wamepoteza maisha wakiwa wanalitumikia Taifa,
naungana na familia za marehemu wote, Jeshi la Polisi na Watanzania wote katika
kipindi hiki kigumu cha huzuni na majonzi ya kuondokewa na vijana wetu shupavu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu atupe moyo wa
subira, uvumilivu na ustahimilivu,” alisema Rais Magufuli katika taarifa hiyo.
Dk. Magufuli pia alilaani tukio hilo na
matukio yote ya kuwashambulia askari Polisi wanaofanya kazi kubwa na muhimu ya
kulinda raia na mali na kuwataka Watanzania wote watoe ushirikiano katika
kukomesha vitendo hivyo.
ACT, CCM
Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi jana
kilituma salamu za pole kwa Mwenyekiti
wa chama hicho, Rais Magufuli kutokana na mauaji hayo ya askari Polisi.
Taarifa ya CCm ilieleza kuwa salamu hizo
ziliwasilishwa kwa Rais Magufuli na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Humphrey
Polepole Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
Akiwa ameambatana na Naibu Katibu Kuu
CCM Tanzania Bara, Rodrick Mpogolo na Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania,
Amina Makilagi, Polepole alisema CCM
imeshitushwa na tukio hilo na kutoa pole hizo.
Alisema askari hao wamekuwa wakifanya
kazi katika mazingira magumu wakati wote kuhakikisha Watanzania wanakuwa salama
pamoja na mali zao hivyo kuuwawa kwao ni jambo la kusikitisha.
Naye Katibu, Kamati ya Amani na Usalama wa chama cha ACT
Wazalendo, Mohammed Babu, aliwataka Watanzania washikamane wakati huu wa majonzi
ya kupoteza askari.
“Chama cha ACT Wazalendo kimepokea kwa
masikitiko makubwa taarifa ya kushambuliwa na kuuawa kwa askari wanane wa Jeshi
la Polisi jana jioni katika eneo la Jaribu Mpakani, wilayani Kibiti, mkoa wa
Pwani.
“Chama cha
ACT Wazalendo kinatoa pole kwa familia za mashujaa wetu hawa wanane waliouawa
wakati wakilinda usalama wetu wananchi, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP
Ernest Mangu pamoja na Jeshi zima la Polisi,” alisema.
Alisisitiza
kuwa ACT Wazalendo wanaungana na kutoa mwito kwa Watanzania kushikamana na
vyombo vya ulinzi na usalama katika kipindi hiki cha majonzi kwa Taifa pamoja
na kutoa ushirikiano kwao kuhakikisha matendo ya namna hii yanakomeshwa.
0 comments:
Post a Comment