Hussein Ndubikile
VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa
kujenga utamaduni wa kuibua mijadala itakayosaidia kuiletea nchi maendeleo huku
vikisisitizwa kuacha kusubiri ajenda za mipango ya maendeleo kutoka kwa wanasiasa.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Theophil Makunga wakati wa
utoaji taarifa ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani
itakayofanyika Mei 2 na 3 Mwanza.
Alisema katika jamii kuna mambo mengi
yanayotakiwa kuibuliwa kwa kuyasemea ili kufanyiwa kazi na mamlaka husika,
hivyo ni vema vyombo hivyo vikajikita kutatua matatizo yanayokabili wananchi.
"Duniani kote, tabia za vyombo vya
habari hubadilika hivyo lazima vyombo vyetu vibadilike, tusigonje ajenda za
wanasiasa zije kwetu, tunatakiwa kugusa matatizo yanayoigusa jamii,"
alisema Makunga.
Alisisitiza kuwa vyombo vya habari
vinatakiwa kuyapa umuhimu matatizo ya kijamii huku akitaka kuitumia siku hiyo
kupiga kelele ya kuhakikisha uhuru wa vyombo hivyo unapatikana.
Aliongeza kuwa nchi zingine suala la
uhuru wa vyombo liko katika hali mbaya na kwamba hali hiyo haitakiwi
kuvirudisha nyuma kuendelea kudai haki hiyo.
Makunga alisema suala la vyombo vya
habari kusubiri ajenda za Serikali lilikuwapo lilipotangzwa Azimio la Arusha na
Azimio la Iringa na kwamba wakati huu waandishi wa habari wanatakiwa kubadilika
kuendana na hali iliyopo.
Awali akizungumzia kuelekea Siku hiyo
ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais John Magufuli, Mwenyekiti wa Taasisi
ya Vyombo vya Habari ya Kusini mwa Afrika (MISA), Salome Kitomari alisema zaidi
ya washiriki 250 wa ndani na nje ya nchi wamealikwa.
Alisema atakuwapo pia Waziri wa Habari, Sanaa,
Michezo na Utamaduni, Dk Harrison Mwakyembe, Wakuu wa Mashirika ya
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya nchini, mabalozi, wabunge, wakuu wa asasi zisizo za serikali za kitaifa,
vyuo vya uandishi wa habari, wanachama wa vyama vya kijamii na waandishi wa
habari wakongwe.
Alifafanua kuwa masuala mbalimbali
yatajadiliwa yakiwamo ya lengo la kufikia makubaliano ya kitaifa kuhusu
utaratibu wa usalama na ulinzi wa wanahabari na wafanyakazi wa vyombo hivyo
kwenye mitandao na nje ya mitandao na kuweka msukumo kwa mataifa kutunga sheria
rafiki za vyombo hivyo zitakazohakikisha uhuru katika nchi husika.
Aidha, alisema wakati wa maadhimisho
hayo, wahanga wa ukiukwaji wa uhuru wa habari watatoa ushuhuda kuhusu
changamoto walizokutana nazo wakati wakitekeleza majukumu yao.
Salome alisema siku hiyo Ripoti ya
vyombo vya habari vya Kusini mwa Afrika iliyoandaliwa na MISA inayojulikana kwa
jina la ‘Kwa hiyo hii ni Demokrasia’ itazinduliwa pamoja na mfululizo wa
taarifa ya UNESCO ya sera za vyombo vya habari vya kijamii.
Mwakilishi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari
(TMF), Razia Mwawanga alisema kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni fikra yakinifu
kwa wakati mwafaka, huku akibainisha kuwa waandishi wanahitaji kufanya kazi zao
bila kuingiliwa.
Alisema Mfuko huo umefanya kazi kubwa ya
kuwezesha waandishi wa habari 40 wa vyombo 13 kuandika habari zilizochangia
uwajibikaji.
Mwakilishi wa Klabu za Umoja wa
Waandishi wa Habari nchini (UTPC), Jane Mihanji alitaka waandishi kuchukua hadhari
wanapokuwa kwenye kazi zenye mazingira hatarishi na kuwasisitiza kuacha
kutumiwa vibaya na wanasiasa.
Mwakilishi wa Shirika la Idadi ya Watu Duniani
(UNDP), Stella Vuzzo alisema siku hiyo ina umuhimu kwa kuwa inatambuliwa na
Umoja wa Mataifa na nchi wanachama wanahamasishwa kuiadhimisha.
0 comments:
Post a Comment