Suleiman Msuya
Benki Kuu ya Tanzania |
SERA za Serikali ya Awamu ya Tano za
kubana matumizi na kuongeza ukusanyaji wa mapato, zimeanza kuathiri ukuaji wa
uchumi ambao unaonekana kushuka badala ya kupanda.
Ripoti ya Benki ya Dunia (WB), kuhusu
hali ya uchumi nchini imeeleza kuwa katika robo ya tatu ya mwaka jana, uchumi
ulishuka hadi kufika asilimia 6.2 kutoka asilimia 7.9 ya robo ya pili ya mwaka
huo.
Waandaaji wa ripoti hiyo
walipolinganisha ukuaji wa uchumi wa robo ya tatu ya mwaka jana na mwaka juzi
walibaini kwamba uchumi umeshuka kutoka asilimia 7.3 hadi 6.2.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo taarifa zake
zinaonesha kwamba mazingira ya ukuaji wa robo ya nne ya uchumi pia ni magumu.
Ripoti hiyo ilitaja sababu kubwa tatu
kuwa ni kudhoofika kwa mazingira ya ufanyaji biashara, kupungua kasi ya utoaji
mikopo na kupungua kwa kasi ya utekelezaji wa bajeti hasa katika miradi ya
maendeleo.
Kutokana na hali hiyo ripoti inaonesha
kuwa ukuaji wa uchumi wa mwaka jana unatarajiwa kuwa asilimia 6.9 pungufu ya
matarajio ya Serikali ya ukauji wa asilimia 7.2.
Ripoti hiyo imeonya kuwa sera za
Serikali tangu kuingia utawala wa Rais John Magufuli hasa katika kupunguza
matumizi ya Serikali, ikitolea mfano katazo la semina za Serikali katika hoteli
binafsi kwamba zinaharibu ukuaji wa sekta binafsi.
Katika hilo ripoti hiyo imefafanua
kwamba sekta binafsi inategemea sana kuhudumia Serikali katika mahitaji ya
huduma na bidhaa na kuonya kuwa sera za kupunguza mahitaji ya huduma na bidhaa
serikalini zitapunguza kazi za sekta binafsi.
Pili imeonya kuwa sera hizo
zikitekelezwa mara kwa mara zitatoa ishara ya hatari kwa sekta binafsi hali
ambayo itasababisha uwekezaji katika sekta hiyo kukwama na hivyo kuathiri
ukuaji wa uchumi kwa siku zijazo.
Aidha, ripoti hiyo imeonya Serikali
kwamba iwe makini katika utekelezaji wa sera kuepuka matokeo hasi ya sera hizo
katika sekta binafsi.
Akifafanua ripoti hiyo mmoja wa
waandaaji kutoka WB, Abebe Adugna alisema katika kuhakikisha kuwa hali hiyo
haitokei Serikali inapaswa kuhamasisha uwekezaji huku ikiweka mazingira rafiki
na wawekezaji.
Alisema pia Serikali inapaswa kuangalia
sekta mbalimbali kama ujenzi, usafirishaji, kilimo na huduma za jamii hasa
katika rasilimali watu ili kuhakikisha kuwa inaweza kukabili changamoto za
kiuchumi ambazo zinaweza kutokea.
“Kiujumla uchumi si mzuri katika nchi
zote za Bara la Afrika kwani takwimu zinaonesha kuwa umeshuka hadi kufikia
asilimia 1.5 ambayo haijawahi kutokea kwa miaka ya hi9vi karibuni,” alisema.
Umaskini
wakithiri
Adugna alisema pia Serikali inapaswa
kuongeza jitihada katika kusaidia familia maskini ambapo Tanzania inaonesha
kuwa zaidi ya Watanzania milioni 12 wanaishi kipato cha chini ya dola moja kwa
siku.
Mkurugenzi Mkazi wa WB katika nchi za
Burundi, Tanzania, Malawi na Somalia, Bella Bird akizungumza kabla ya uzinduzi
wa ripoti hiyo ya tisa ya hali ua uchumi nchini alisema uchumi wa Tanzania bado
uko imara pamoja na kutoongezeka ikilinganishwa na nchi za Jangwa la Sahara na
Afrika Mashariki.
Alisema ripoti hiyo ya tisa imejikita
katika muktadha wa kuimarisha sekta ya fedha nchini ili kuamsha midahalo kutoka
kwa wadau na wanafalsafa kuhusu uchumi wan chi.
Bird alisema wao kama WB wameangalia
katika maeneo mbalimbali ambapo
alisisitiza kuwa uchumi wa Tanzania umeonesha ustahimilivu katikati ya ukuaji
unaosuasua katika nchi za ukanda wa Afrika Kusini mwa Sahara.
“Uchumi wan chi hizi ulishuka hadi
kufika asilimia 1.5 kiwango kibaya zaidi kuweza kutokea kwa zaidi ya miaka 20
na visababishi kutoka nje ndio sababu kubwa,” alisema.
Aidha, alisema wakati bei za biadhaa
zikibaki kuwa chini, chumi nyingi zinazotegemea rasilimali zimehangaika
kudhibiti matokeo ya mshituko wa biashara.
“Kinyume chake Tanzania imebaki moya ya
chumi tatu katika Afrika ya Kusini mwa Sahara pamoja na Rwanda na Ethiopia
ambazo zinaendelea kuonesha ustahimilivu katika mazingira yenye changamoto,”
alisisitiza.
Mkurugenzi mkazi alisema nafasi ya
Tanzania kiuchumi ipo imara huku akitahadharisha kuwa hakuna nafasi ya
kubweteka ili kuweza kufikia asilimia 7 ya ukuaji au 10 ifikapo mwaka 2020/21
ili kufikia uchumi wa viwanda.
Bird alisisitiza kuwa kufikia viwango
hivyo inawezekana iwapo idadi ya wananchi wanaishi chini ya mstari wa maskini
itaondolewa na kuajiri zaidi ya vijana 800,000 ambao wanaingia katika soko la
ajira.
Aidha alishauri Serikali kuendelea na
sera makini ya uchumi, umuhimu wa uwekezaji wa umma na kuendeleza na kusisimua
ukuaji wa siku zijazo na kutengeneza ajira kwa kufungulia uwezo wa sekta
binafsi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.
Ashatu Kijaji alisema ripoti inaonesha Tanzania inafanya vizuri na kuahidi
kuongeza juhudi zaidi hasa katika kutekeleza miradi mbalimbali.
Alisema ripoti imeonesha changamoto
kubwa ipo katika kupata fedha kutoka nje jambo ambalo anakiri kuwa lipo na kuwa
wamejipanga kukabiliana na hali hiyo.
Kuhusu sekta binafsi kushuka alisema
hayo ni mambo ambayo yanatokea katika Serikali mpya na kwamba wao wamejipanga
kufanya kazi nao kwani bila wao ni vigumu kufukia Tanzania ya viwanda bila
sekta hiyo.
0 comments:
Post a Comment