Grace Gurisha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam
imelazimika kuahirisha kesi ya mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam ‘Pedeshee
ndama mtoto wa Ng’ombe, Hussein Ndama (44), kwa sababu Wakili wa Serikali
anayeendesha kesi hiyo hakuwepo mahakamani.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 27, mwaka huu, baada
ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shedrack Kimaro kumueleza Hakimu Mkazi
Victoria Nongwa wa mahakama hiyo kuwa wakili aliyetakiwa kujibu hoja
zilizowasilishwa na upande wa utetezi anaumwa, kwa hiyo aliomba kesi
iahirishwe.
Upande wa Jamhuri waliwasilisha hoja kuwa hati ya
mashtaka ya mfanyabiashara huyo ina upungufu wa masuala ya kisheria, kwa hiyo
mahakama iitupilie mbali hati hiyo na mshtakiwa aachiwe.
Ndama anakabiliwa na makosa sita likiwemo la kutakatisha
fedha haramu na kujipatia dola za Marekani 540,390 sawa na zaidi ya Sh. bilioni
moja kwa njia ya udanganyifu na jana alipandishwa kizimbani akiwa amefungwa
pingu, jambo ambalo liliwashangaza ndugu, jamaa na marafiki.
Ndama ambaye anatetetewa na Wakili Hashimu Rungwe anashtakiwa
kuwa Februari 20, 2014 akiwa Dar es Salaam kwa nia ya kudanganya alighushi hati
ya uongo ya kuuza madini nje na sampuli ya madini kwa kuonesha Kampuni ya Muru
Platnum Tanzania Investment Ltd imemruhusu kusafirisha maboksi manne ya dhahabu
yenye uzito kilogramu 207 yenye thamani ya dola za Marekani 8,280,000.00 zaidi
ya Sh. bilioni 16 huku akijua si kweli.
Katika kosa la pili, mshtakiwa huyo anatuhumiwa kuwa Machi
6, 2014 akiwa Dar es Salaam alighushi
hati ya uongo inayotoka ofisi za Umoja wa Mataifa zilizopo Dar es Salaam ya
Machi 16, 2014 kwa kuonesha kuwa kilo 207 za dhahabu kutoka Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo ambazo zinatarajiwa kusafirishwa na Kampuni Muru kwenda
Kampuni ya Trade TJL DTYL Ltd iliyopo Australia na kwamba zimesafirishwa bila
jinai yoyote.
Ilidaiwa kuwa Februari 20, 2014 alighushi nyaraka
ya malipo ya yenye namba R. 28092 ya Februari 20,2014 kwa kuonesha
Kampuni ya Muru imelipa kodi ya dola za Marekani 331,200 Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) kwa ajili ya uingizwaji wa kilo 207 za dhahabu zenye thamani ya
dola za Marekanin 8,280,000 zilizokuwa zinatoka Congo huku akijua si kweli.
Ndama anatuhumiwa kuwa Februari 20, 2014 alighushi bima
kutoka Kampuni Phoenix of Tanzania Assurance Ltd ya tarehe hiyo kuonesha
Kampuni Muru imewekea bima maboksi manne ya dhahabu huku akijua si kweli.
0 comments:
Post a Comment