*Aeleza tofauti ya Ukapa na kusoma namba
*Asema haukudumu muda mrefu kama sasa
Celina Mathew
Frederick Sumaye |
WAZIRI Mkuu wa Serikali ya Awamu ya
Tatu, Frederick Sumaye, amechambua tofauti ya mazingira ya utawala wa awamu ya
tatu, ambao ulikuwa na changamoto ya kukosekana kwa fedha na kinachotokea sasa
maarufu kusoma namba.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na
gazeti hili jana, Sumaye alisema kuna tofauti nyingi lakini akaamua kuzungumzia
kubwa zaidi kwa kujikita katika mambo mawili; moja ni uchumi na lingine
demokrasia na utawala bora.
Sumaye ambaye ndiye Waziri Mkuu mwenye
historia ya kukaa miaka kumi mfululizo katika nafasi hiyo, alisema katika Awamu
ya Tatu Serikali iliimarishwa uchumi na kukuza na kuboresha nguzo kuu za uchumi,
kwa kujenga mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na kuingiza ushindani wa kweli
katika biashara.
Kwa mujibu wa Sumaye ambaye sasa ni kada
wa Chadema, Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais Benjamin Mkapa, ndiyo iliyojenga na kubuni vivutio kwa
wawekezaji wa ndani na wa nje na kuanzisha ushirikiano wa sekta ya umma na
binafsi (PPP) katika uwekezaji.
Sumaye aliendelea kueleza kuwa Awamu ya Tatu,
ambayo hali yake ya kukosena kwa fedha ilipewa jina la ‘Ukapa’ ndiyo iliyobuni
na kuboresha miundombinu ya uchumi kwa kuunda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
na Kituo cha Uwekezaji (TIC) pamoja na kuboresha sheria zilizoendana na uchumi
huria na wa kisasa.
Alisema hata maboresho ya miundombinu ya
barabara, bandari na maji yalianzia Awamu ya Tatu na katika huduma za jamii
hasa elimu, awamu hiyo ndiyo iliyobuni Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya
Msingi (MMEM), uliopeleka watoto wote wenye umri wa kuanza shule
darasani na Mpango wa
Maendeleo ya Elimu Sekondari (MMES).
“Awamu hii mengi ya mambo haya ni
kinyume kabisa au hayatiliwi mkazo. Kwa mfano Serikali imekwishatamka kuwa
kuanzia mwaka huu wa fedha idara za Serikali hazitapewa huduma na sekta
binafsi. Hii ni kinyume kabisa na sera ya PPP,” alisema.
Alisema hata sera ya utozaji kodi,
inapaswa kujenga uhusiano mwema baina ya mlipakodi na mtozakodi, lakini cha
kushangaza hazishabihiani na badala yake wafanyabiashara wengi wamefunga
biashara zao.
Upatikanaji wa fedha
Akizungumzia hali ya upatikanaji fedha
iliyopewa jina la ‘Ukapa’, Sumaye alisema Awamu ya Tatu ilipoanza, hali ya
uchumi ilikuwa duni na fedha zilikuwa mikononi mwa wenye uchumi usio rasmi au
uchumi wa magendo.
Alisema kazi ya kwanza ya Awamu Tatu,
ilikuwa kurudisha uchumi katika misingi sahihi na katika kufanya hivyo
walikubaliana kuua biashara ya magendo.
Alieleza kuwa kipindi hicho ndiyo watu
wengi walipoona ugumu wa fedha kupatikana wakauita 'Ukapa', lakini kipindi
hicho hakikudumu muda mrefu, kwani uchumi ulirudi katika misingi bora na
kuimarika na watu wakaanza kupata fedha kulingana na jasho lao halali.
Demokrasia
Sumaye alisema Awamu ya Tatu pia ilikuza
demokrasia na utawala bora na idadi ya vyama iliendelea kukua na vyama vya
siasa vilifanya kazi za kisiasa kwa uhuru bila kuzuiwa au kungiliwa.
Alifafanua kuwa utawala bora wakati wa Awamu
ya Tatu, ulikuwa wa 'ukweli na uwazi na uliofuata sheria’ na kutolea mfano wa
nguzo tatu za dola ambazo ni Utawala, Bunge na Mahakama kwamba zilifanya kazi
kwa uhuru bila nguzo moja kuingilia nyingine.
Waziri Mkuu huyo alisema watu walikuwa
huru kutoa maoni yao bila wasiwasi wala kamata kamata au watu kupotea bila
maelezo yoyote kutoka vyombo vya dola.
“Awamu hii ni kinyume kabisa na hivyo.
Demokrasia imekandamizwa kiasi kwamba vyama siasa havina uhuru wa kufanya
mikutano ya hadhara kama sheria inavyotaka na uhuru wa vyombo vya habari
umeminywa kabisa. Mikutano ya Bunge haioneshwi tena mbashara katika luninga
kama zamani,” alisema.
Aliongeza kuwa hayo yote yanavunja Katiba
ya nchi ibara ya 18 kwa sababu ni haki ya kikatiba wananchi kuwa na uhuru wa
kutoa, kupata au kusambaza habari.
Alisema kwa sasa ni jambo la kawaida
wapinzani kukumatwa bila sababu za msingi na kukaa rumande muda mrefu kuliko
saa 48 zinazoruhusiwa kisheria na hata wengine kufungwa jela.
Kwa mujibu wa Sumaye, hata kupotea kwa watu
wenye mawazo tofauti na Serikali au 'kuvamiwa na watu wasiojulikana' kumeanza
kuwa jambo la kawaida.
0 comments:
Post a Comment