Mwandishi Wetu
Tundu Lissu |
MNADHIMU wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu,
amesema baadhi ya maneno ya hotuba za kambi hiyo kuzuiwa kusomwa bungeni ni
kinyume na kanuni za mhimili huo wa Dola.
Mbunge huyo wa Singida Mashariki amesema kwa mujibu wa
kanuni hizo, inatakiwa msomaji hotuba kuachwa asome kwanza ndipo aelezwe kuwa
baadhi ya maneno aliyosoma ni kinyume na kanuni, si kumzuia kusoma maneno
yaliyomo.
Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Rais
wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) alitoa kauli hiyo zikiwa zimepita siku
mbili tangu Msemaji wa Upinzani wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na
Muungano, Ally Salehe kususa kusoma hotuba yake ya upinzani kuhusu wizara
hiyo.
Salehe alilazimishwa kuacha kusoma baadhi ya maneno
yakiwamo yanayohusu Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar na mgogoro wa CUF.
Hali hiyo ilitokea baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), George Masaju kusimama na kupinga baadhi ya maneno aliyotumia kama
“kila wizara imekiona cha moto, wamebanwa mpaka wamevunjwa mbavu” na kuwa Ofisi
ya Makamu wa Rais imeathirika vibaya na kisu cha ngariba kwa kukata bajeti
yake.
Baada ya malumbano, Mwenyekiti wa Bunge, Musa Zungu
alitoa uamuzi kuwa maneno yaliyoandikwa
kuanzia ukurasa wa tatu hadi wa saba kwenye hotuba hiyo yasisomwe wala
kurekodiwa kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge.
Kauli hiyo ilimfanya Salehe kutoendelea kusoma hotuba
yake na yaliyobaki anamwachia ngariba afanye anavyotaka.
Akizungumza na gazeti hili, Lissu ambaye hotuba yake ya Wizara
ya Katiba na Sheria ilipingwa na AG kutokana na kuwa na dosari, alisema hotuba
ya Salehe haikurekodiwa, sambamba na yake kutokana na uamuzi wa Kiti cha
Spika.
“Kwa kilichotokea, maana yake hotuba hairekodiwi. Hata
yangu sijui kama imerekodiwa, ngoja nisubiri nione kama wataniletea
marekebisho. Wasiponiletea maana yake haijarekodiwa,” alisema Lissu.
“Mambo yanayofanyika kwenye Bunge la Tanzania ni ya
kigeni, hatujawahi kuyaona kwa kweli. Huu utaratibu wa kuzuia watu kusoma
hotuba zao ni utaratibu mpya na haupo kwenye kanuni kabisa,” alisisitiza.
Alisema juzi wakati akisoma hotuba ya kambi hiyo ya
Wizara ya Katiba na Sheria AG na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na wenye Ulemavu, walimkatisha kwa zaidi ya dakika
15 lakini muda wake haukulindwa na Kiti.
Alisema licha ya kuwa maneno hayo yanazuiwa, lakini
kiundani wanalenga kuwasilisha ujumbe stahiki ikiwa ni pamoja na kuikosoa na
kuishauri Serikali.
0 comments:
Post a Comment