*Wasiwasi watanda nani leo nani kesho
*Wengi
washangaa ukimya wa Serikali
Waandishi
Wetu
KWA takribani miezi sita sasa, Taifa
linatikisika kutokana na hofu iliyotanda miongoni mwa wananchi kwa matukio ya uvamizi
na watu maarufu kutekwa kiasi cha kutojua nani aliye salama kila uchwao au nani
atafuata uchao.
Hali hiyo imeibua wasomi ambao wameieleza
JAMBO LEO kwamba Serikali inatakiwa kuunda tume ya uchunguzi kubaini ukweli wa
matukio ya utekaji, wakieleza kuwa wajibu wake ni kulinda usalama wa raia na
mali zao.
Tangu Agosti mwaka jana hadi jana zaidi
ya matukio 10 ya utekaji na uvamizi yameripotiwa na vyombo vya habari
yakihusisha watu mbalimbali, wakiwamo wanasiasa, wanahabari, daktari na wasanii.
Matukio hayo yameliteka pia Bunge
linaloendelea Dodoma na mitandao ya kijamii ambako yanajadiliwa na wananchi huku
baadhi ya wabunge wakiituhumu Idara ya Usalama wa Taifa kuhusika.
“Hivi sasa kila mtu ana hofu mitaani.
Wananchi hawajui nani atatekwa kesho. Serikali ijitathmini na kuchukua hatua,
maana hali hii imezidi kwa kweli. Inanishangaza Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa
kimya. Kwa nini hatoi kauli kuwatoa hofu wananchi?” Alihoji Richard Mbunda,
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Hii maana yake Serikali imeshindwa
kufuata mkataba namba moja kwa raia wake ambao unaitaka kuwalinda na mali zao.
Mkataba huu huingiwa tu pale wananchi wanapochagua Serikali,” aliongeza.
Matukio
Kutoweka kwa Mkuu wa Idara ya Sera na
Utafiti wa Chadema, Ben Saanane tangu Agosti 8 mwaka jana, kulianza kuibua
maswali mengi, huku wanasiasa, hasa wa Upinzani wakivitaka vyombo vya ulinzi na
usalama kufuatilia aliko msaidizi huyo wa
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Wakati sakata hilo likiwa halijapoa,
Machi 23 aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
alitishiwa bastola, muda mfupi kabla ya kuzungumza na wanahabari kueleza hatua
ya Rais John Magufuli kumwacha katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.
Akizungumzia tukio hilo, Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema aliyemtishia bastola Nape si polisi,
lakini hakueleza ni nani.
Nape aliondolewa siku moja baada ya
kupokea ripoti ya uchunguzi wa tukio la kiongozi mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kuvamia
kituo cha televisheni cha Clouds Media, akiwa na askari wenye silaha za moto na
kulazimisha arushiwe mahojiano baina ya watangazaji wa kipindi cha Shirika la
Umbea Duniani (Shilawadu) na mwanamke anayedai kuzaa na Askofu wa Kanisa la
Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ambaye ameibuka kuwa mpinzani wa kiongozi
huyo wa mkoa.
Machi 26, msanii Emmnuel Elibariki ‘Ney
wa Mitego’ alikamatwa na polisi akiwa Morogoro baada ya kutoa wimbo wa ‘Wapo’
ambao unaeleza uwepo wa watu wa aina tofauti katika jamii, wakiwamo viongozi
wenye vyeti vya kughushi na kuuliza sababu za ‘jipu lililoiva kutotumbuliwa’.
Ney aliachwa na polisi baada ya Rais
Magufuli kusema anaupenda wimbo huo.
Aprili 5, mwanamuziki ‘Roma Mkatoliki’
na wenzake watatu wakiwa katika studio za Tongwe, Dar es Salaam, walitekwa na
watu wasiojulikana, tukio ambalo limezua maswali mengi kutokana na Waziri
anayehusika na Sanaa, Dk Harrison Mwakyembe kuibuka kwenye mkutano wa
mwanamuziki huyo na wanahabari.
Roma ambaye nyimbo zake nyingi zimekuwa
na mashairi ya kuikosoa Serikali, alionekana siku tatu baadaye katika kituo cha
Polisi Oysterbay, ambako alikwenda kuripoti tukio hilo.
Juzi, Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi
Hillary (CCM) alieleza bungeni kuwa ni muda mrefu hajaingia Dar es Salaam, kwa
sababu alitishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo, akidai
wabunge wamezidi unafiki, na kwamba katika kuwashughulikia ataanza naye.
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe
(CCM) alitoa ushuhuda kuwa ni mmoja wa waliotekwa na Usalama wa Taifa na kwamba
yuko tayari kuvuliwa uanachama kwa kusema ukweli.
Wakati Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto
Kabwe (ACT) akieleza mbele ya Bunge juzi kuhusu kutoweka kwa Saanane sambamba
na ushahidi alionao kuwa Usalama wa Taifa unahusika, Tume ya Serikali ya Haki
za Binadamu (THBUB) ilikemea matukio hayo ya utekaji.
Wachambuzi
“Kwa nini Tume isiundwe? Inaonekana
watekaji hawa si watu wa kawaida. Si majambazi hawa kwamba wanateka watu ili
wapate fedha. Inaonekana ni kikundi kinachofanya kazi maalumu.
“Tume itatueleza ni akina nani hawa watekaji.
Kama ni vyombo vya ulinzi na usalama vinahusika basi tujue,” alisema Profesa
Gaudence Mpangala, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco).
Alisema Serikali inatakiwa kujitathmini
kama inapaswa kuendelea kuwa madarakani kutokana na kushindwa kutoa tamko
lolote juu ya matukio ya uvamizi na utekaji yanayoendelea nchini.
Katika ufafanuzi wake, Mpangala alisema Serikali
ina njia nyingi za kupambana na watu wenye nia mbaya kutokana na kuwa na vyombo
vya ulinzi na usalama, huku akishangazwa na ukimya uliopo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino
(Saut), Profesa Mwesiga Baregu aliungana na Profesa Mpangala akitaka kuundwa
tume ya uchunguzi.
“Wabunge pia wamependekeza jambo hili,
nadhani ndicho kitu kinachopaswa kufanyika sasa. Tume hii ndiyo itatupa majibu
sahihi,” alisema.
“Ni kama inavunja mkataba wake na
wananchi wa kuwalinda kwa hali yoyote ile. Haiwezekani wasiwe na upande wa
kusimamia. Haiwezekani Tanzania kuwa na matukio ya utekaji ambayo tumezoea
kuyaona katika nchi za Mexico, Honduras na Colombia,” aliongeza.
0 comments:
Post a Comment