*Mmoja alidanganya askari wakampa ufunguo
*Wadakwa wakigawia karatasi wanafunzi 15
Costantine
Mathias, Simiyu
WALIMU wawili wa
sekondari za Nyawana na Shishani wilaya ya Bariadi na Itilima mkoani hapa wamehukumiwa
kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja kwa kosa la kuiba na kuvujisha mtihani wa
Taifa wa kidato cha nne.
Walimu
waliohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Simiyu, ni Issa Makene
(40) wa sekondari ya Shishani na Solela Mangura (26) mwalimu wa kujitolea wa
sekondari ya Nyawana, ambaye hata hivyo hakuwa mahakamani wakati hukumu
ikitolewa jana kutokana na kuruka dhamana na kutokomea kusikojulikana tangu
kesi yake itajwe mwaka 2013.
Awali akiwasomea
mashitaka yao katika kesi namba 176/2015, kabla ya hukumu kutolewa na Hakimu
Mkazi wa Mahakama hiyo, mwendesha mashitaka wa serikali, Moses Mafuru alidai
tukio hilo lilitokea Novemba 10, 2013, katika sekondari ya Sagata.
Mafuru alidai
kuwa Mwalimu Makene akiwa Mkuu wa Kituo cha Mitihani cha sekondari ya Sagata,
siku ya tukio wakati wa chakula cha usiku aliwalaghai askari waliokuwa
wakilinda mitihani katika kituo hicho.
Aliendelea kudai
kuwa Makene aliwaomba askari hao wampe ufunguo wa chumba kilichohifadhi mitihani
hiyo na baada ya kupewa, alifungua chumba na kwenda moja kwa moja kwenye kabati
lenye mitihani hiyo.
Mafuru alidai
kuwa mara baada ya kufungua kabati mtuhumiwa, alichukua bahasha lenye mtihani
wa somo la Fizikia kisha kwenda kuuficha chini ya uvungu wa kitanda chake shuleni
hapo.
Alidai kuwa
kesho yake baada ya mwalimu huyo kuchukua bahasha Novemba 11, 2013 aliichana na
kutoa karatasi moja ya mtihani huo na kumkabidhi mwalimu Solela.
Halikadhalika, walimu
hao walikuwa kwenye harakati za kuwapa wanafunzi 15 wa shule hiyo ambao
mwendesha mashitaka aliwataja kuwa ni Abasi Makwaya, Veronica Jonathan,
Mboji Masike, Saka Masuki, Milembe Mabula, Makula Saya na Prisca Jonathan.
Wengine ni
Getruda Senga, Buye Masike, Msafiri Samson, Japhet Martine, Alex Jackson na
Khamis Nkwabi.
Akisoma hukumu, Hakimu
John Nkwabi aliamuru washitakiwa hao kwenda jela miaka 20 kila mmoja, kwa kuwa
Mahakama ilijiridhisha na ushahidi ulitolewa na upande wa mashitaka.
Kuhusu hukumu
hiyo, Ofisa Elimu wa Mkoa, Julius Nestory alisema haki imetendeka na kuwa
fundisho kwa walimu wengine, huku akibainisha kuwa hajafurahia kufungwa kwa
walimu hao.
Aliwataka walimu
hao kukata rufaa kama wanaona hawajatendewa haki, huku akiwataka wengine kuwa
na nidhamu kazini kwa kufuata sheria na kanuni za utumishi wa umma, ikiwa ni pamoja
na wanaopangiwa kusimamia mitihani kuachana na vitendo hivyo.
0 comments:
Post a Comment