*Kamati ya Ulinzi na Usalama yateta faragha na mawaziri
Joyce Kasiki, Dodoma
TUKIO la mauaji ya askari wanane
lililotokea wiki iliyopita wilayani Kibiti mkoani Pwani, jana liliwalazimisha wabunge
wakiongozwa na Spika Job Ndugai kutaka chombo hicho cha kutunga sheria
kuahirisha shughuli zake siku hiyo ili wajadili mauaji hayo.
Walifikia uamuzi huo, baada ya
kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu asubuhi.
"Mimi niungane na waheshimiwa wote
mlioonyesha kuguswa sana na suala hili la askari wetu kuuawa na kufikia wanane,
wakati mmoja kuuawa kwa kweli ni jambo linalosikitisha. Kwa hiyo kwa niaba ya Bunge
zima ningependa kutoa pole na rambirambi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na
kipekee kwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa jambo hili kubwa ambalo limetushtua
wote katika nchi yetu." alisema Spika Ndugai akiunga mkono hoja za
wabunge.
Awali, mbunge wa Bukombe Dotto Boteko
(CCM) alisema Aprili 13 katika Kijiji cha Makengeni, Rufiji, askari wanane waliuawa
na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi na kwamba askari hao walikufa wakati wakitekeleza
majukumu ya kulinda raia na mali zao.
Alisema tukio hilo siyo la kwanza, huku
akikumbusha tukio lingine lililotokea wilayani Kibiti mkoani Pwani Februari 21
mwaka huu ambapo watu watatu waliuawa, akiwemo mkuu wa upelelezi Wilaya ya Kibiti,
Peter Kubeza.
"Kama askari hawapo salama kwa
kiwango hiki, raia wa kawaida hali yao ikoje?| alihoji Biteko na kuongeza:
“Jambo hili limetokea Kibiti, lakini
linaweza kutokea Kongwa, Bukombe hata mahali kwingine kokote na kama Taifa
halijachukua hatua madhubuti ni hatari.
Naomba tuahirishe shughuli za Bunge tujadili
jambo hili moja, ili Bunge kama chombo cha uwakilishi wa wananchi kije na kauli
ya kuitaka Serikali kutoa kauli ya kueleza kwa nini mambo haya yanaendelea
kujitokeza na Serikali wakati wote inatoa kauli lakini matukio hayo yanaendelea
kujitokeza."
Mbunge wa Mtambile Masoud Abdallah Salim
(CUF) aliomba busara ya Spika Ndugai itumike ili wabunge wajadili suala hilo
ambalo limetia hofu kwa wananchi.
Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel
(CCM) aliungana na wajumbe waliotangulia, huku akikazia kwa kunukuu Ibara ya 14
ya Katiba.
Akijibu miongozo hiyo, Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema Serikali inalichukulia tukio hilo kwa
uzito mkubwa ili kuhakikisha wanarejesha hali ya usalama katika maeneo hayo na
nchi nzima kwa jumla kama alivyoeleza Waziri Mkuu katika kauli yake aliyoitoa
hivi karibuni.
Nchemba alitumia fursa hiyo kuwatoa hofu
wananchi na kusema kuwa tukio hilo limewapa chachu zaidi ya kupambana na
uhalifu katika kuhakikisha wananchi wanakuwa katika mazingira salama wao na
mali zao.
Kamati
ya ulinzi na usalama
Katika kuonyesha uzito wa tukio hilo, Kamati
ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Ulinzi na Usalama nayo jana ilipanga kukutana
mchana baada ya kuahirishwa kwa shughuli za Bunge asubuhi.
Kikao hicho pia kilihusisha mawaziri
wenye dhamana ili kupata taarifa rasmi kuhusu matukio hayo.
Ndugai alisema kamati hiyo itaeleza
namna ilivyojipanga ili kuyakabili matukio mengine yanayoweza kujitokeza na
kuhatarisha hali ya usalama ya polisi na mali zao .
0 comments:
Post a Comment