Is-haka Omar, Zanzibar
Dk Shein |
BAADHI
ya waasisi wa ASP, wasomi na viongozi wa Serikali na kidini jana waliudhuria
maadhimisho ya kumbumbuku ya Mashujaa Zanzibar na kuzungumzia umuhimu wa mikakati
iliyoachwa na Hayati Mzee Abeid Aman Karume, kuwekwa kisheria ndani ya Katiba
ya Zanzibar.
Walieleza
kwamba miongozo na fursa za kiuchumi, kijamii na kimaendeleo ilichoachwa na
Mzee Karume inayotekelezwa sasa, haitoshi kubakia katika Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya mwaka 2015/2020.
Kwa
mujibu wa wasomi hao, kuwekwa kwa miongozo hiyo katika Katiba ya Zanzibar ya
mwaka 1984, kutailazimisha Serikali yoyote itakayoongoza nchi, itekeleze kwa
vitendo.
Akizungumza
baada ya Dua ya hitima ya maadhimisho ya kumbukumbu ya mashujaa ambao ni
waasisi wa ASP, waliokomboa Zanzibar toka utawala wa Kisultani, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema Mzee Karume, ameacha
urithi wa hazina ya fikra na mawazo ya maendeleo yanayotakiwa kuendelezwa na
vizazi vya sasa na vijavyo.
Majaliwa
alisema katika miaka nane ya utawala wa Kiongozi huyo, aliwatoa wananchi kwenye
giza la uonevu na mateso na kuwaweka kwenye mwanga wa mafanikio ya kimaendeleo,
yanayoendelezwa kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Saba Zanzibar kwa
kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed akitoa
nasaha zake kwa wananchi, aliwasihi kuendelea kuunga mkono Serikali iliyopo
madarakani kwani ndiyo inayosimamia na kutekeleza, fursa zilizoachwa na waasisi
wa ASP waliowekewa siku maalum ya kitaifa kukumbukwa kwa kusomewa dua kutokana
na juhudi zao za kukomboa nchi.
Alisema
Zanzibar itaendelea kuimarika kiuchumi endapo kila mwananchi bila ya kujali
itikadi za kisiasa na kidini, atalinda amani, utulivu na kuchukia kwa vitendo ubaguzi,
kama ilivyokuwa kwa mashujaa wa ASP walivyoondosha utawala wa mabavu.
“Leo
tumeadhimisha kumbukumbu ya mashujaa wetu lakini bado tuna kazi kubwa ya
kulinda na kuendeleza urithi wa wazee wetu, kwani bado zipo choko choko za
baadhi ya watu wenye nia ya kuchafua amani ya nchi yetu, lakini na sisi wajue
tupo imara kama wazee wetu walivyokuwa mashujaa na kutetea maslahi ya wanyonge,”
alielea Waziri Aboud.
Mwenyekiti
wa Chama Cha Wakulima (AFP) Zanzibar, Said Soud Said amesema kazi
aliyofanya Mzee Karume ndio iliyozaa matunda ya Wazanzibari kuishi kwa utulivu
na kujiamulia mambo yao wenyewe.
Alisema
ukombozi wa Zanzibar wa mwaka 1964 aliousimamia yeye ndio hasa kioo cha
Wazanzibari duani nzima kujiona kuwa wapo huru na wenye uwezo wa kujenga Taifa
lao kiuchumi bila vikwazo vyovyote.
Soud
ambaye pia ni Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, alisema baada ya mapinduzi hayo Mzee Karume aliweka
misingi iliyofuatwa na viongozi waliotawala baada yake ambayo kwa sasa wananchi
wote wa Zanzibar wananufaika nayo.
Asha
Simba Makwega aliyelelewa na Mzee Karume na baadae akawa kada wa ASP, alisema
kiongozi huyo alitumia muda wake kushughulikia kero na matatizo ya wananchi,
kuliko muda alioutumia kwa familia yake, hali inayothibitisha uzalendo na
utaifa wa kweli wa shujaa huyo.
0 comments:
Post a Comment