Grace Gurisha
Sengodo Mvungi
|
WAKAZI sita wa Dar es Salaam wanaotuhumiwa kumuua kwa
makusudi aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi, leo
wanatarajiwa kusomewa maelezo ya mashahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.
Washitakiwa hao ni John Mayunga (56), Juma Kangungu (29),
Longishu Losingo (29), Paulo Mdonondo
(30), Mianda Mlewa (40) na Msungwa Matonya (30).
Maelezo hayo yanatarajiwa kusomwa na Wakili wa Serikali,
Patrick Mwita mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa Mahakama hiyo, ambapo
washitakiwa hao waliposomewa mashitaka ya mauaji walikana kuhusika.
Baada ya kusomewa maelezo yao, jalada la kesi hiyo
litapelekwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ili kesi ianze
kusikilizwa, kwa sababu Mahakama ya Kisutu kisheria haina mamlaka ya kusikiliza
kesi hiyo.
Awali, Mwita aliieleza Mahakama kuwa hawawezi kuwasomea
maelezo hayo, kwa sababu bado wanashughulikia taratibu za kuliondoa jina la
Chibago Magozi kwenye jalada ambalo lipo Mahakama Kuu, kwa sababu bado
hawajapata cheti cha kifo licha ya kuandika barua kwa mamlaka husika.
Awali, washitakiwa walikuwa 11 mmoja akafariki dunia na
kubaki 10, na kati yao Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Biswalo Mganga aliwasilisha
mahakamani nia ya kutoendelea kuwashitaki wanne kwa hiyo wakabaki sita.
Washitakiwa walioachwa huru baada ya kusota rumande kwa miaka
minne ni Ahmed Kitabu (30), Zacharia Msese (33), Masunga Makenza (40) na
Msungwa.
Inadaiwa kuwa washitakiwa hao Novemba 3, 2013, wakiwa Msakuzi Kiswegere, Kinondoni, kwa pamoja
walimuua Dk Mvungi.
0 comments:
Post a Comment