Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Chakula na Dawa Tanzania
(TFDA) imewataka wananchi kuendelea kutumia mafuta ya alizeti yaliyothibitishwa
nayo.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya
habari na Mkurugenzi wa TFDA, ilisema imefanya uchambuzi wa awali wa matokeo ya
utafiti uliofanywa mwaka 2014/15 na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Michigan,
Marekani kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuhusu
mafuta hayo.
Ilisema utafiti huo ulihusu mbegu za
alizeti na mashudu kuchafuliwa na sumukuvu aina ya Aflatoxins, hivyo vyombo vya
habari juzi kutoa hadhari kwa watumiaji.
“TFDA imefanya uchambuzi wa awali wa
matokeo ya utafiti huo na kubaini kwamba ulihusu mbegu za alizeti na mashudu
pakee na hivyo hautoshelezi kuthibitisha kuwa mafuta ya alizeti yamechafuliwa
na Aflatoxins kwa kiwango ambacho ni hatarishi,” ilisema taarifa.
Hata hivyo, TFDA ilisema itafanya uchambuzi
wa kina wa matokeo ya utafiti yaliyochapishwa kwenye jarida la PLOS One na
kufanya ufuatiliaji na uchunguzi zaidi wa mbegu, mashudu na mafuta ya alizeti
yaliyozalishwa nchini.
“Mwito unatolewa kwa watafiti nchini
wanaofanya utafiti kuhusu usalama na ubora wa chakula, dawa, vipodozi,
vifaatiba na vitendanishi, kushirikisha TFDA kama mdau muhimu juu ya matokeo ya
utafiti wao ili yatumike kuimarisha mifumo ya udhibiti na hivyo kulinda afya ya
jamii,” ilifafanua taarifa hiyo.
Vyombo vya habari vilishauriwa pia
kuwasiliana na TFDA kupata maoni na tafsiri sahihi kuhusu matokeo ya utafiti wa
kisayansi kuhusu usalama wa chakula, dawa, vipodozi, vifaatiba na vitendanishi,
kabla ya kuchapisha ili kuondoa uwezekano wa kuleta hofu kwa jamii.
0 comments:
Post a Comment