Mwandishi Wetu
BUNGE la Bajeti linaendelea leo Dodoma
huku kukiwa na kila dalili za wabunge ‘kuwasha moto’, hali inayoweza kuibua
mvutano mkali kutokana na ‘madudu’ yaliyotajwa katika Ripoti ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.
Licha ya kuwa wiki hii kunatarajiwa bajeti
ya Ofisi ya Rais na ya Makamu wa Rais zitawasilishwa, hilo haliwezi kuwaondoa
wabunge katika mjadala wa ripoti hiyo ambayo Serikali haiwezi kukwepa
kuwajibika kushughulikia yaliyotajwa.
Ripoti hiyo imeanika ‘madudu’ kila kona,
huku deni la Taifa likizidi kupaa na kueleza namna vitendo vya ukwepaji kodi
katika taasisi mbalimbali za Serikali ikiwamo migodi ya dhahabu ambayo
haijalipa kodi kwa miaka 10.
Jambo la kwanza ni ushauri uliotolewa na
Profesa Assad kuhusu bajeti iliyopita jinsi ilivyotekelezwa ambapo aliishauri
Serikali kupanga bajeti inayoweza kuitekeleza, badala ya kupanga kiasi kikubwa
ambacho hakina uhalisia.
CAG alitoa kauli hiyo huku takwimu za
Wizara ya Fedha zikieleza kuwa hadi Februari mwaka huu, fedha zilizokuwa
zimetolewa kwa ajili ya maendeleo ni Sh trilioni 3.97 kati ya Sh trilioni 11.8
zilizopitishwa na Bunge Juni mwaka jana kugharimia miradi mbalimbali ya
maendeleo.
Hivi karibuni, Mbunge wa Kigoma Mjini,
Zitto Kabwe (ACT) alisema alisema wabunge wanapoteza muda kukaa bungeni Dodoma
kujadili bajeti hiyo aliyodai ni kiini macho.
Kwa mujibu wa Zitto, bajeti ya kwanza ya
Serikali ya Awamu ya Tano (2016/17) imeonesha upungufu mkubwa katika utekelezaji
na kwamba baada ya kupitia taarifa zilizowasilishwa na Waziri wa Fedha, Dk
Philip Mpango kwenye Kamati za Bunge za kisekta alibaini kuwa bajeti ya 2016/17
ilipaswa kuwa Sh trilioni 24.8 na si Sh trilioni 29 iliyowasilishwa na Serikali
Juni mwaka jana.
Mbali na bajeti, jambo jingine
linaloweza kuzua mjadala ni taarifa ya uchunguzi ya Mei, mwaka jana kubaini
matumizi mabaya ya msamaha wa kodi wa Sh bilioni 3.46 ambao ulitolewa kwa
walengwa wawili walioagiza magari 238. Magari hayo yalisajiliwa kwa majina
tofauti na waliopewa msamaha huo.
Jambo lingine ni jinsi ukaguzi
ulivyobaini lita 20,791,072 za mafuta yenye msamaha wa kodi wa Sh bilioni 10.17
kwa ajili ya mgodi wa Buzwagi kwa miezi 18 yalivyosafirishwa kwenda kampuni ya
M/S Aggreko na mkandarasi msaidizi ambaye hakuwa mhusika katika msamaha huo.
Wakati sakata la vitambulisho vya Taifa
likiwa linafukuta, kwenye ripoti ya CAG imebainishwa jinsi ukaguzi
ulivyojiridhisha kuwa uongozi na watoa huduma na wazabuni walivyoshiriki kwa
namna moja au nyingine katika ubadhirifu na udanganyifu kwenye matumizi ya
fedha katika mradi wa kuboresha vitambulisho vya Taifa.
Mambo mengine yatakayotikisa chombo
hicho cha kutunga sheria ni ucheleweshwaji wa fedha za michango ya hifadhi za
jamii, Tanesco kupata hasara, kushuka kwa mapato ya uwekezaji kwa kiasi kikubwa
kwenye mifuko ya pensheni ya NSSF, PPF, PSPF na LAPF.
Ushuru wa Sh bilioni 15 ulioyeyuka
bandarini, malipo ya mishahara ya Sh bilioni 7.3 na makato ya kisheria ya Sh
bilioni 2.5 yaliyofanyika kwa watumishi walioacha kazi au kufariki dunia ,
Serikali kutokarabati ofisi za balozi za Tanzania nje ya nchi sambamba na
Tanesco kuwa mteja pekee anayetumia gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment