Fidelis Butahe
Zitto Kabwe |
WAKATI Bunge la
Bajeti likianza leo Dodoma, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto
Kabwe amesema kitendo cha wabunge kukaa bungeni kwa miezi mitatu kujadili Bajeti
ya Mwaka 2017/18 ni sawa na kupoteza muda.
Zitto ambaye pia
ni Mbunge wa Kigoma Mjini alidai jana kuwa bajeti hiyo ya Sh trilioni 31.6
haiwezi kutekelezeka, akirejea alichokiita uongo wa utekelezaji wa Bajeti
iyobakiza miezi mitatu kumalizika, akisisitiza kuwa ya sasa haitatekelezwa
zaidi ya Sh trilioni 28.
Aliwataka
wabunge kuhoji utekelezaji wa Bajeti ya 2016/17 na kutaka ichambuliwe kwa kina
kuonesha hali halisi na kuitaka Serikali iandike upya Bajeti inayopendekezwa ya
mwaka 2017/18.
“Wabunge
wasikubali matumizi ya kawaida kuitwa ya maendeleo. Mfano, mwaka huu ili kuonesha
Bajeti ya Maendeleo ni kubwa, Serikali imerundika matumizi kama kununua dawa, fedha
za ruzuku zinazokwenda shuleni na maeneo mengine na kuziita za maendeleo,”
alisema.
Alitoa kauli
hiyo takribani siku tano tangu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango
kuwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango
cha Ukomo wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Katika maelezo
ya Dk Mpango, Serikali ilitoa theluthi moja tu ya fedha zilizotengwa kwa ajili
ya mwaka 2016/17 huku mwaka ujao wa fedha ikipanga kukusanya na kutumia Sh
trilioni 31.6 ikilinganishwa na Sh trilioni 29.5 za Bajeti ya mwaka huu, huku
uwiano wa bajeti ya maendeleo ukishuka hadi asilimia 38 kutoka 40 ya mwaka
jana.
Dk Mpango
alisema hadi Februari mwaka huu, fedha zilizokuwa zimetolewa kwa ajili ya
maendeleo ni Sh trilioni 3.97 kati ya Sh trilioni 11.8 zilizopitishwa na Bunge
Juni mwaka jana, kugharimia miradi ya maendeleo.
Katika taarifa
yake aliyoituma kwa vyombo vya habari jana, Zitto alisema: “Ni dhahiri Tanzania
inakwenda kupoteza muda wa miezi mitatu kujadili Bajeti nyingine ambayo ni ya
kujidanganya. Bajeti halisi ya 2017/18 haitazidi Sh trilioni 28. Tulisema
kwenye Bajeti ya 2016/17.”
Kwa mujibu wa
Zitto, bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano (2016/17 ) imeonesha upungufu
mkubwa katika utekelezaji na kwamba baada ya kupitia taarifa zilizowasilishwa
na Dk Mpango kwenye kamati za Bunge za kisekta, alibaini kuwa Bajeti ya 2016/17
ilipaswa kuwa Sh trilioni 24.8 na si Sh trilioni 29 iliyowasilishwa na Serikali
Juni mwaka jana.
“Mpaka Machi, lengo
la makusanyo ya mapato yote ya Serikali limeshindwa kufikiwa kwani ni asilimia
79 ya makusanyo ndiyo imekusanywa,” alisema.
“Hata kama
Serikali itakusanya asilimia 100 kwa miezi yote iliyobaki hadi Juni 2017 bado
lengo halitafikiwa kwa sababu kuna vyanzo Serikali imesema haitaweza kabisa
ikiwamo mikopo ya kibiashara kutoka nje.”
Alisema Serikali
imesema rasmi haitapata Sh trilioni 2 kutoka mikopo ya kibiashara, kwamba lengo
la makusanyo litafikia asilimia 90 na hivyo kukosa Sh trilioni 1.7.
Alisema hata
wafadhili wataongeza fedha hadi asilimia 80 (sasa wametoa asilimia 40 ya lengo),
na hivyo kukosa Sh trilioni moja.
“Kwa hiyo Bajeti
halisi itakuwa Sh trilioni 24.8 tu. Haya ni makisio ya juu kabisa na ni
ongezeko linaloeleweka kulinganisha na bajeti ya Sh trilioni 22.9 aliyoiacha
Saada Mkuya Salum (aliyekuwa Waziri wa Fedha) mwaka 2015/16,” alisema.
Alihoji sababu
za Serikali kuleta Bajeti ya Sh trilioni 31.7 wakati Bajeti ya 2016/17
imeshindwa kufikiwa, “ Hili ndio swali kila mbunge makini anajiuliza hapa
Dodoma. Serikali inataka kuzitoa wapi fedha za Bajeti mpya?”
Akifafanua
kushindikana kutekelezwa kwa Bajeti hiyo, Zitto alisema mapato ya kodi ya
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni Sh trilioni 17 kutoka Sh trilioni 15 za
sasa ambazo hazitafikiwa kwa kiasi cha Sh trilioni 1.5, yaani asilimia 90 ya
lengo la mwaka 2016/17.
“Mapato yasiyo ya
kodi Sh trilioni 2.2 ambapo kwa sasa chanzo hiki kimefikia asilimia saba tu ya
lengo la 2016/17. Mapato ya halmashauri ni Sh trilioni 0.7 ambapo kwa sasa
chanzo hiki kimefikia asilimia 70 tu ya lengo la 2016/17,” alisema.
“Mikopo na misaada
nafuu kutoka nje ni Sh trilioni 4 ambapo chanzo hiki kimefikia asilimia 40 tu ya
lengo la 2016/17. Mikopo ya ndani na yenye masharti ya kibiashara ni Sh
trilioni 8 ambapo chanzo hiki kimefikia asilimia 78 ya lengo la mwaka 2016/17.”
0 comments:
Post a Comment