Suleiman Msuya
Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema
Tanzania itafikia uchumi wa viwanda iwapo nidhamu ya kazi, ubunifu, elimu na
matumizi makubwa ya sayansi na teknolojia vitapewa kipaumbele.
Aidha, alisema Serikali inahitaji
kuimarisha sekta binafsi, miundombinu ya huduma za kiuchumi na jamii na kuondoa
urasimu usio wa lazima.
Waziri Mkuu huyo aliyasema hayo wakati
akiwasilisha hotuba ya kuhusu mapitio na Mwelekeo wa kazi za Serikali na Makadirio
ya Mapato na Matumizi ya fedha za ofisi yake bungeni mjini Dodoma kwa mwaka
2017/2018 mwishoni mwa wiki.
Alisema mafanikio yoyote katika kujenga
uchumi wa viwanda yataonekana kupitia misingi ya nidhamu kuanzia kwa
wasimamizi.
Alisema anafarijika kwamba misingi wanayoendelea
kujenga katika kutekeleza azma hiyo imeanza kuzaa matunda.
Waziri Mkuu huyo alisema kuwa ustawi wa
nchi na mafanikio ya mipango ya maendeleo vinategemea amani na utulivu hivyo,
kila Mtanzania anapaswa kuweka nadhiri ya kuendelea kuilinda na kuienzi amani
ya nchi ili mipango iweze kufanikiwa.
Alisema jukumu la kujenga uchumi wa nchi
ni wajibu wa kila mwananchi, hivyo jamii inapaswa kufanya kazi kwa bidii,
kulipa kodi kwa hiari na kufichua wakwepa kodi wote na wala rushwa.
“Ujenzi wa uchumi wa viwanda unahitaji
wananchi wenye afya njema na maarifa ya kufanya kazi na ubunifu. Tujenge utamaduni wa kupima afya zetu na
kufanya mazoezi ya viungo ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo
yanapoteza nguvu kazi kubwa ya Taifa,” alisema.
Majaliwa alisema rasilimali zilizopo ipo
siku zitaisha hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuzitumia kwa uangalifu na kuepuke
matumizi mabaya ya rasilimali kama vile maji, madini na misitu ili zinufaishe
kizazi hiki na vizazi vijavyo.
Aidha, aliomba jamii na watumishi kuongeze
nidhamu na uwajibikaji katika kila jambo la maendeleo linalolifanyika na
kuzingatia matumizi ya muda na kuachana na tamaduni na mila zinazohamasisha
uvivu na uzembe.
Majaliwa alitoa rai kwa kila mwananchi
kutoa ushirikiano katika vita ya dawa za kulevya kwa kufichua mtandao wa
wahusika.
0 comments:
Post a Comment