Mwandishi Wetu
Respicius Timanywa |
MKURUGENZI wa shirika lisilo la serikali la Kupunguza
Umasikini na Kutunza Mazingira (APEC), Respicius Timanywa, ameomba wananchi
kutoa taarifa za mtu au tukio wanalotilia shaka ili kukomesha uhalifu nchini.
Timanywa alitoa mwito huo hivi karibuni, kutokana na
tukio la uhalifu lililosababisha mauaji ya askari wanane Kibiti mkoani Pwani,
wakati akizungumza na madereva wa bodaboda Dar es Salaam kwa kuwahamasisha kulaani
mauaji ya polisi.
Mkurugenzi huyo aliwataka wajenge utamaduni wa kujikinga
na majanga kwa kuhakikisha wanatoa taarifa kwa wakati, ambapo aliwaeleza kuwa
kwa kazi wanayoifanya ni wepesi sana kupata taarifa kirahisi kutokana na
mizunguko yao.
Alisema tukio la mauaji ya polisi wanane lililotokea
Aprili 13, Mkengeni kata ya Njawa wilayani Kibiti, Pwani lilifanywa na wahalifu,
ambao inasadikika wananchi wanatambua maficho yao kwa sababu matukio kama hayo yamekuwa
kwenye maeneo hayo kwa muda mrefu.
Alibainisha kuwa wananchi wanatakiwa kujitambua kwa kutoa
taarifa za uhalifu mapema, kwa sababu kama zingetolewa mapema na kwa wakati,
askari hao wasingepoteza maisha.
"Mafunzo ya kuwajengea uelewa wananchi juu ya umuhimu
wa polisi na vituo vya Polisi yatolewe kupitia mradi wa mafunzo ya usalama
barabarani, ulinzi shirikishi na ujasiriamali kwa waendesha bodaboda unaoendelea
kutekelezwa nchini," alisema Timanywa.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha
kutambua kuwa ulinzi na usalama ni wajibu wa kila Mtanzania, hivyo kila mtu mwenye taarifa, tukio au mtu anayemtilia
shaka apeleke taarifa Polisi mara moja.
“Mbali na Polisi pia mtoe taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa
Kata, uongozi wa kijiji, mtaa au Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi au Mkuu wa Sekondari,
lengo liwe ni kutokomeza mauaji,” alisema.
Pia aliomba waendesha bodaboda 350,000 waliopewa mafunzo
ya usalama barabarani na shirika hilo nchini, kuzindua kampeni ya kulaani mauaji
ya polisi na kuhamasisha wananchi kuwa ni wajibu wao kuwakinga.
0 comments:
Post a Comment